October 19, 2013


Wakati mwingine umewadia wa kuonyesha soka ya Tanzania imekuwa ikirejea nyuma badala ya kupiga hatua.

Zinapokutana Simba na Yanga, ndiyo siku sahihi ya kuonyesha utamaduni wa mpira wa Tanzania kuwa timu hizo mbili ndiyo kubwa.

Timu hizo zinakutana kesho Jumapili katika mechi ya Ligi Kuu Bara huku kila moja ikiwa imepania kushinda, lakini kila kitu kinaonekana kwenda kisiasa, mfumo wa kizamani na mengi yanayopewa nafasi, hakuna sehemu duniani ambako mpira umeendelea yangeweza kupata nafasi hata chembe.

Kipindi hiki ndiyo utaona namna watu wanavyofanya mambo nje ya utaalamu wa soka, mambo yanakwenda tofauti kabisa na mpira unavyotaka.
Wanachama waliobandika jina la Ukomandoo bila ya mafunzo, kuna fedha zinatolewa kibao kwa ajili ya kwenda kwa waganga wa kienyeji na kuna timu kwa kila timu imekuwa ikifanya kazi hiyo, sasa ndiyo wakati mwafaka wa kufaidika bure.
Lakini utasikia wazee wa Yanga au Simba wakipewa nafasi kubwa kuzungumzia timu kwamba itashinda, wakati hawajui lolote kuhusiana na maandalizi badala ya timu.
Unapomsikia mzee wa Yanga au Simba anasema masuala ya kiufundi, ni sehemu ya kuonyesha kiasi gani ubabaishaji wa mambo unapofikia mchezo wa watani hao huchukua nafasi kubwa.
Ajabu zaidi, kuanzia jana jioni kumekuwa na tangazo kwamba uongozi wa Yanga umeitisha mkutano wa viongozi wa matawi ya Yanga, Baraza la wazee na Kamati ya utendaji ili kupanga mikakati ya kuifunga Simba.
Inawezekana Simba wamefanya hivyo pia kimyakimya, lakini kama hawatakuwa wamefanya, basi huenda wamejifunza na sasa wanapiga hatua kimawazo.
Bora Yanga ingewakaribisha wachezaji wake wa zamani kuzungumza na wachezaji kuhusiana na mchezo, au kufanya kitu tofauti na hicho.
Au uongozi ungetumia muda mwingi kuzungumza na wachezaji na makocha ambao ni benchi la ufundi kwa kuwa wao ndiyo wanajua kuhusiana na mchezo huo na nini cha kufanya.
Viongozi wa matawi au wazee, wanapanga mikakati ipi ya kuifunga timu nyingine. Soka linachezwa uwanjani, wao watakuwa jukwaani. Au ndiyo kwenda kwa waganga?
Siasa inapitiliza katika soka huku tukitangaza kuwa tunataka kufika mbali kimaendeleo na kila siku tunaangalia Ulaya.
Hujawahi na haitatokea kusikia Arsenal inayaalika matawi yake kwenda kuzungumza kuifunga Manchester United, au Chelsea kufanya hivyo iifunge Manchester City au Liverpool.
Tunataka kufikia huko waliko akina Manchester, lakini tunaendelea kukumbatia utamaduni mchovu wa enzi zile. Lazima tubadilike, hakuna ujanja kinachofanyika sasa ni kupoteza muda.

Propaganda zisiwe ubora wa mechi za soka Tanzania, badala yake mambo ya ufundi, waachiwe benchi la ufundi. Ndiyo maana timu ikifanya vibaya huwa wanaofukuzwa ni makocha. Kama viongozi wa matawi na wazee wanahusika katika hilo, timu ikiboronga mbona huwa hawawajibiki?

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic