Na Saleh Ally
Uongozi wa Simba umeanza juhudi za
kusaka mshambuliaji mwingine raia wa Burundi ambaye umepewa taarifa zake kwamba
ni hatari katika upachikaji wa mabao.
Kama Simba itampata Mrundi huyo
ambaye bado hajawekwa wazi, basi mara moja itaachana na Mganda, Moses Oloya,
ili kuongeza nguvu ya upachikaji mabao katika safu ya ushambuliaji ya kikosi
cha Abdallah Kibadeni.
Mrundi Amissi Tambwe anaongoza kwa
kupachika mabao kwenye Ligi Kuu Bara na sasa anayo nane baada ya kucheza mechi
saba.
Mfungaji bora wa msimu uliopita
alikuwa ni Kipre Tchetche wa Azam, raia wa Ivory Coast, sasa dalili zinaonyesha
huenda mfungaji bora atakuwa ni Mrundi au Mtanzania.
Kabla ya raia huyo wa Ivory Coast,
Wakenya na Waganda wamekuwa wakiwasumbua Wabongo kwa ufungaji. Huenda
mabadiliko yakatokea lakini sasa ushindani ni dhidi ya Warundi.
Wakati Tambwe anaongoza akiwa na
mabao nane, anayemfuatia ni Themi Felix wa Kagera Sugar mwenye mabao manne.
Baada ya hapo, anafuatia Mrundi
mwingine, Didier Kavumbagu wa Yanga mwenye mabao matatu, sawa na Watanzania
wengine Jerry Tegete (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Paul Nonga (Mbeya City),
Peter Michael (Prisons) na Bakari Kondo (Ruvu Shooting).
Katika soka chochote kinaweza
kubadilika na mwenye mabao nane anaweza akafikiwa au vinginevyo, lakini mwendo
wa Tambwe kama atakuwa na afya njema, basi kuna kazi kwa kuwa ana mambo kadhaa ambayo
mshambuliaji anapaswa kuwa nayo.
Pamoja na kasi, lakini hesabu za
kuwahi pasi, yaani sehemu sahihi katika wakati mwafaka ni kubwa sana. Angalia
mshambuliaji mwingine wa Simba anapopiga shuti kwenye lango pinzani. Mara
nyingi Tambwe hufuatilia.
‘Urafiki wake na kipa’ ni mara kwa
mara na anatumia mfumo wa “binadamu na makosa”. Mara nyingi hachezi mbali na kipa hasa kunapokuwa
na purukushani langoni, anajua linaweza kufanyika kosa naye akaukwamisha mpira wavuni.
Tatizo kubwa alilonalo ni nguvu,
mwenyewe amekubali kwamba anahitaji muda kuzoea uchezaji wa nguvu wa Ligi Kuu
Bara.
Lakini wako wenye nguvu kama Felix,
ambapo uwezo wake wa kupambana na mabeki ni mkubwa. Pia anapiga mashuti ingawa
anapungukiwa kasi kama ile ya Tambwe.
Kavumbagu ni kati ya washambuliaji
wasumbufu sana kwa mabeki na huwa hachoki.
Kweli ni ‘roho ya paka’ lakini anakosa kasi ya kutosha. Katika mashuti
si mzuri sana lakini pia ana uwezo mkubwa wa kutoa pasi za mwisho kwa wenzake.
Nonga pia ni kati ya washambuliaji
wenye nguvu na mashuti, mzuri wa mipira ya juu kama ilivyo kwa Kavumbagu. Anaweza
kuwa mmoja wa washambuliaji bora zaidi kama atapata uzoefu. Lakini ni tatizo
kubwa la mabeki na mara nyingi anajitahidi kuwa katika sehemu husika.
Chanongo yeye ni kiungo, anapiga
mashuti makali, ana kasi lakini bado hana uwezo mzuri wa kulenga goli. Mabao
aliyofunga yanaonyesha atakuwa tishio baadaye, tayari Kocha Mkuu wa Taifa
Stars, Kim Poulsen, ameliona hilo, amekuwa akimchezesha namba kumi katika
kikosi chake badala ya pembeni.
Ukiangalia namna washambuliaji hao
wanavyoongoza msimamo wa wapachika mabao, inaonyesha wazi ushindani utakuwa mkubwa
na wapo watakaoondoka na kuachwa nyuma huku wapya wakipanda nafasi za juu,
ambao sasa wana bao moja au mawili tu.
Tambwe
KASI 89%
PASI 82%
TAIMINGI 95%
MASHUTI 75%
NGUVU 60%
Felix
KASI 78%
PASI 79%
TAIMINGI 80%
MASHUTI 90%
NGUVU 85%
Kavumbagu
KASI 78%
PASI 75%
TAIMINGI 80%
TAIMINGI 80%
MASHUTI 85%
NGUVU 80%
Chanongo
KASI 91%
PASI 76%
TAIMINGI 68%
MASHUTI 80%
NGUVU 82%
Tegete
KASI 80%
PASI 70%
TAIMINGI 93%
MASHUTI 75%
NGUVU 75%
Fin.
0 COMMENTS:
Post a Comment