Kipa namba moja wa Yanga, Ally
Mustapha ‘Barthez’, amejikuta akiwa katika wakati mgumu, baada ya kupata
taarifa mbaya juu ya kuvamiwa nyumbani kwake na mashabiki wanaodhaniwa kuwa ni
wa Yanga.
Barthez ambaye ni kipa namba moja wa
Yanga amekuwa akituhumiwa kuwa alicheza chini ya kiwango kwenye mchezo wa Ligi
Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Simba, baada ya timu yake kuongoza kwa mabao 3-0
lakini mechi ikamalizika kwa 3-3.
Jana asubuhi, zinasema kuwa watu hao
ambao walikuwa kundi kubwa, walifika nyumbani kwa kipa huyo, maeneo ya Chanika
jijini Dar, na kuanza kumsaka kipa huyo, lakini wakapewa taarifa kuwa yupo
kambini.
Mara baada ya kuelezwa kuwa hayupo,
watu hao ambao walionekana kuwa na hasira na kipa huyo waliondoka eneo hilo
huku majirani wakitazama kwa mbali kuona nini kitakachotokea.
Hata hivyo, baada ya Barthez ambaye
ni kipa wa zamani wa Simba kujulishwa kuhusu tukio hilo lilitokea usiku wa
kuamkia jana aliondoka na kwenda kuihamisha familia yake na kuipeleka mafichoni
baada ya kuelezwa kuwa watu hao wamepanga kurudi tena.
“Hawakuwa wastarabu kabisa, walikuja
hapa na kutaka kumfanyia vurugu, walikuja wengi wengine wakiwa na silaha,
bahati nzuri hawakumkuta.
“Unajua awali nasikia Barthez
mwenyewe alishajulishwa na wasamaria wema, kuwa kuna mpango wa watu kutaka
kumfanyia fujo, hivyo akaihamisha familia yake,” alisema shuhuda mmoja.
Kuhusiana na hilo Barthez, ambaye
alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema anachoshukuru ni kutodhurika kwa
familia yake na kusema yote anamuachia Mungu na uongozi wa klabu yake
kulishughulikia.
“Hizo taarifa ni kweli, nashukuru
Mungu familia yangu ilisalimika, siwezi kuongea chochote zaidi, binafsi nasema
namwachia Mungu na uongozi wa klabu kulishughulikia, ingawa limenifanya
nichanganyikiwe kidogo,” alisema Barthez, aliyekuwa mnyonge mithili ya mtu
aliyeua.
0 COMMENTS:
Post a Comment