Katika kile kilichoonekana kukosekana
kwa ustaarabu, mashabiki wa Yanga, wamefanya kihoja cha mwaka, baada ya kuibuka
katika mazoezi ya timu hiyo na kuanza kuwashushia matusi wachezaji wa timu
hiyo.
Tukio hilo lilitokea jana asubuhi,
wakati Yanga ikijifua katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola, Mabibo,
Jijini Dar, chini ya kocha wao Mholanzi Ernie Brandts, ambapo wakati kikosi
hicho kikiendelea na mazoezi hayo, waliibuka mashabiki hao wakiwa nje ya uzio
wa uwanja huo na kuanza kuwashushia matusi makali wachezaji hao.
Wakati mashabiki hao wakifanya hivyo,
wachezaji wa Yanga walionyesha utulivu mkubwa kwa kuvumilia huku wakiendelea na
mazoezi, lakini uvumilivu ulifikia kikomo, ambapo kitendo cha sekunde nne,
zilitosha kwa wao kujikusanya na kukubaliana kuwafuata mashabiki hao na
kuanza kuwafukuza huku wakiwatupia mawe.
Hakuna hata shabiki mmoja, aliyeweza
kuvumilia kasi ya mawe, ambapo wote walitimua mbio kali mithili ya wanariadha
na kuondoka katika uwanja huo, ndipo wachezaji hao waliporudi na kuendelea na
mazoezi, huku kocha wao Ernie Brandts, akionyesha kuchukizwa na hali hiyo.
Mara baada ya kumalizika kwa mazoezi
hayo, Brandts alizungumzia tukio hilo, ambapo alikuwa mkali kwa mashabiki hao
huku akiwataka kuacha kuwasumbua wachezaji hao, akitaka aachiwe yeye ndiye
ashughulikie kiufundi, yote yanayotokea katika kikosi hicho.
“Sijawahi kuona tukio kama hili,
mashabiki kuwatukana wachezaji tena wakiwa mazoezini, nafikiri uongozi kuna
kitu unatakiwa kukifanya, hata kama wamefanya makosa lakini siyo ya kuja
mazoezini na kuanza kuwatukana, waniachie mimi ndiyo najua nini nifanye juu ya
yale yaliyotokea katika mechi,” Alisema Brandts.
Tukio hilo linakuja kufuatia kikosi
hicho cha Yanga kutoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya watani wao Simba, Jumapili
iliyopita, ambapo matokeo hayo yanaonyesha kuwakera mashabiki wengi wa klabu
hiyo.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment