October 23, 2013



Aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Davis Mosha amesema kimefika kipindi ambacho atapumzika kidogo kufanya kazi zake kama shabiki wa timu hiyo na badala yake kulitumikia taifa.

Mosha amekuwa akisifika kama jembe la mipango ya ushindi Yanga, ameamua kuelekeza nguvu katika michezo kwa ujumla.

Mosha anasema uamuzi huo unatokana na kwamba amechukua fomu kugombea uongozi katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).


“Nitagombea ujumbe wa TFF kupitia mikoa miwili ya Kilimanjaro na Tanga. Kutokana na hali hiyo, nalazimika kutokuwa upande mmoja tu, yaani Yanga. Sasa nitalitumikia taifa kwa jumla na nguvu nitaelekeza Kilimanjaro na taifa zima kwa jumla,” anasema Mosha katika mahojiano maalum.

Mosha anayemiliki malori zaidi ya 200 kupitia kampuni yake ya Delina Group Ltd, anaamini kuna mambo mengi ambayo yanakwamisha mpira wa Tanzania na vijana wenye upendo na michezo na wanaoweza kujitolewa wanaweza kufanya vizuri wakipewa nafasi.

Kujitolea:
Kujitolea ni jambo muhimu sana, hamuwezi kukaa halafu ukasikia hakuna mipira katika kambi ya timu ya taifa na wote mkaanza kulia. Au ukaelezwa Sh milioni 10 zimepungua mkaanza kuhaha. Kinachotakiwa ni kutoa na kufanya mambo yaendelee.

Hapa ishu si watu wenye uwezo, lakini ni watu wanaoweza kujitolea. Unaweza ukawa nacho na usitoea, hivyo lazima tuwe na mapenzi na taifa letu.

Bado ninaamini Tanzania inaweza kufika mbali kama itakuwa na watu wanaotaka iendelee na hili haliwezi kuwa rahisi tu.

Kilimanjaro:
Tokea ilipoondoka Ushirika mwaka 1992 au 93, hadi leo hakuna timu ya ligi kuu kule Moshi. Pale kuna vipaji vingi lakini hamasa na mtu wa kuamsha mambo amekosekana.

Lakini siwezi kupigana kwa ajili ya Kilimanjaro pekee, nimekuwa mpambanaji kuhakikisha michezo inakuwa katika mikoa kama Pwani ambako nilifanya kazi katika kamati ya kuisiadia Pwani kushinda. Bado nikawa na Moro United, lakini kazi yangu Yanga inajulikana.

Niko tayari kupigania maendeleo ya nchi nzima kama nitapewa nafasi na watu wakaniunga mkono. Napenda mpira, ninapenda uendelee maana hakuna sababu ya wengine kuendelea na sisi tunaporomoka tu.

Yanga:
Siwezi kujiondoa Yanga, nitabaki kuwa mwanachama, lakini naona kwa sasa ni bora kujitanua zaidi na kusaidia maisha ya michezo kwa nchi nzima. Mimi ni Mtanzania mwenye uchungu na nchi yangu, kama michezo ikiendelea, basi hata Yanga nitakuwa nimeisaidia.

Familia:
Familia yangu ni muhimu sana, lakini kila kitu kina muda wake. Unajua mimi siendi klabu, sinywi pombe na muda mwingi nakuwa katika michezo na hasa soka, hiyo ndiyo burudani yangu.
Hata familia inalijua hilo, kwamba burudani kubwa kwangu ni michezo. Hivyo inaniachia muda wangu katika michezo.
Utaona tokea Kombe la Dunia mwaka 2002, Japan na Korea, sijawahi kukosa tena. Nasafiri karibu kila nchi duniani sababu ya mpira, ninaona mengi na ninatamani kuona mafanikio hayo yako hapa nyumbani pia.

Chelsea & Madrid:
Nilimpeleka mwanangu kufanya majaribio katika timu za watoto za Chelsea na Real Madrid. Hakika nimejifunza mengi sana na nimezungumza nao kama wanaweza kuanzisha shule za watoto hapa.
Wenyewe wanataka mtu mwenye uwezo ambaye atakuwa tayari kuwekeza fedha zake pia na si wao tu watoe kila kitu. Tayari nimeishanunua eka 100. Naendelea kukubaliana nao na wakikubali, basi mara moja tutaanzisha shule zao hapa nchini.

Vipaji:
Vipaji vikikuzwa, inakuwa rahisi kuwa na wachezaji wa uhakika, nikiwa Chelsea nimeona watoto kuanzia miaka mitatu wanapata mafunzo ya soka.
Hapa utaona tunawalaumu sana wachezaji wengi kwamba tabia zao si nzuri, lakini makuzi yao ndiyo hasa wanavyoishi tofauti na wenzetu. Kuondoa hilo, basi tuwasaidie kwa kuwakuza katika mazingira ya kisoka tokea wadogo.

Magari:
Kweli ninamiliki magari mengi, nina wazimu wa magari. Unajua kazi yangu ni usafirishaji, Kampuni ya Delina Group inamiliki zaidi ya malori 200, nina vituo vya kuuzia mafuta pamoja na kampuni ya kuuza bodi za magari.
Mimi ni mjasiriamali, nikiona biashara nzuri, basi nahamia huko ila magari ya kutembelea ni wazimu kweli, napenda magari mazuri ndiyo maana namiliki kama hiyo Lamborghini, Lexus, Mercedes Benz SL 65, Range Rover na mengine, lakini hivi ni kati ya vitu ninavyopenda.

Kufaidika:

Kweli wako viongozi wanaoingia katika michezo wakitaka kufaidika binafsi, mimi siko huko, michezo ndiyo burudani yangu, nataka ifanikiwe na mimi niwe chanzo au sehemu ya mafanikio hayo. Ndiyo maana nimeingia na kuamua kugombea TFF ili nitoe mchango wangu, hakuna zaidi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic