Uongozi wa Klabu ya Simba umesema kuwa
hautalipa faini ya Sh milioni 25 iliyotokana na mashabiki wa timu hiyo kung’oa
viti kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar hadi hapo mahakama itakapotoa maamuzi
juu ya kesi inayowakabili baadhi ya wanachama wake wanaodaiwa kuhusika.
Simba ilitakiwa kulipa kiasi hicho na
serikali kutokana na vurugu zilizotokea uwanjani hapo wakati wa mechi ya Ligi
Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar iliyomalizika kwa sare ya 1-1.
Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga amesema
kuwa wanasubiri mahakama itakavyotoa hukumu juu ya mashitaka yanayoyakabili
wanachama wao ambao walitajwa kuhusika katika vurugu hizo.
“Hatuwezi kulizungumzia suala hili kwa
kuwa lipo chini ya mahakama, hivyo tutalizungumzia hadi hapo litakapotolewa
hukumu kwani kufanya hivyo ni kuingilia uhuru wa mahakama.
“Hatuwezi kulipa kiasi hicho chote kwa
sasa kwani kiasi ambacho tunatakiwa kukilipa serikalini ndicho hicho
tunachotakiwa kulipa mahakamani, hivyo hatuwezi kulipa fedha zote hizo,” alisema
Kamwaga.
Mashabiki 11 wa Simba walikamatwa
kufuatia vurugu za uwanjani hapo na kufunguliwa kesi.
0 COMMENTS:
Post a Comment