Na Saleh Ally
Kuna ule msemo kwamba unaweza kuwalaghai
watu kwa kipindi fulani, lakini si kila siku.
Binadamu wengi ni welevu lakini wakati
mwingine hudanganywa kutokana na uvumilivu au kuamini kwamba mtu fulani
anayefanya kitu ambacho si sahihi anaweza kujirekebisha.
Inapofikia wamechoka, basi huwa hakuna
ujanja tena na waliosubiri siku zote huwa na msimamo mkali baada ya subira
kwisha nguvu.
Mashabiki na wanachama wa Simba wameanza
kuonyesha njia kwamba hawafurahishwi na mwenendo wa klabu yao chini ya
Mwenyekiti Ismail Aden Rage.
Siku moja tu baada ya kamati ya utendaji
ya Simba kumsimamisha mwenyekiti huyo, yeye alijibu mapigo kwamba atarejea.
Watu wengi walijua na kutangaza, kasha wakashadadia
kwamba Rage atapokelewa na mamia ya watu kwenye uwanja wa ndege na kisha
atakwenda klabuni na kuwapa ‘makavu’ waliomsimamisha.
Lakini mambo yamekuwa tofauti kabisa,
angalia idadi ya waliojitokeza kumpokea Rage kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius
Nyerere, jijini Dar.
Waangalie wao kwanza, utagundua ni
vijana wa aina gani, kwamba wanaonekana wazi walikusanywa kwa ajili ya zoezi
hilo.
Hata baada ya kuingia kwenye magari yao
matatu waliyokwenda nayo uwanjani pale huku yote yakiwa yamepungukiwa watu,
walianza kulalama kuhusiana na posho zao.
Idadi ndogo ya watu hao, ni dalili
kwamba Simba wamechoka, wameanza kuamka na wanaona namna gani mwenendo wa timu
yao ulivyo.
Wako wanaomtetea Rage, kweli wana haki
kwa kuwa pia wanaangalia maslahi yao binafsi.
Lakini wanaotetea maslahi ya klabu yao,
kamwe hawawezi kufanya hivyo tena.
Sasa ni dalili tosha ya muonekano wa
ukweli kuanza kuchukua nafasi yake, kuwaacha nyuma wale waliokuwa wakiamini kwa
kulishwa maneno na sasa watu wataruhusu vichwa vyao vifanye kazi na kutafakari.
Achana na blogu zilizolaghai watu kwamba
Rage alipokelewa na mamia ya wanachama, kitu kilichokuwa uongozi mtupu kwa
lengo la kutaka kumfurahisha mtu mmoja au kikundi kidogo cha watu wachache au
kwa maslahi ya mhusika, yaani mwenye blog.
Ukweli ulionekana, picha zimeonyesha na
hata Rage mwenye alijaribu kuuliza kama kweli klabuni palikuwa salama kabla ya
kupita.
Hii pia ni nafasi nyingine kuona kwamba
mambo yanakwenda tofauti na Simba wengi sasa wameamka na wanataka mabadiliko.
Ukweli usigeuzwe kuwa vibaya, vitisho
vikawa msingi badala yake kama mna hoja, hasa mnaomtetea Rage, basi tuendelee
kubadilishana hoja na si kutaka kutisha watu na mambo kibao kama risasi,
tindikali, huo ni upuuzi mtupu.
0 COMMENTS:
Post a Comment