November 1, 2013


Mapato yaliyotangazwa kupatikana katika mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Mbeya City dhidi ya Tanzania Prisons yamezua gumzo na kuelezwa kuwa ni kidogo tofauti na idadi ya mashabiki walioingia kwenye Uwanja wa Sokoine kuishuhudia mechi hiyo.


Taarifa iliyotolewa na Katibu na Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya (Mrefa), Haroub Seleman ni kuwa mapato yaliyopatikana ni Sh milioni 31.6, kutokana na tiketi 10,558 kati 20,000 zilizotumwa na bodi ya ligi.

Mashabiki waliozungumza na Champion Ijumaa wamesema kuwa idadi hiyo ya mapato iliyopatikana ni ndogo tofauti na mashabiki waliojitokeza. “Mbona idadi ya mashabiki haikutofautiana sana na ile ya mechi ya Mbeya City na Yanga, ambapo mapato yalikuwa makubwa zaidi,” alisema shabiki mmoja.

Akizungumzia hilo, Katibu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe alisema: “Hapa kuna mkanganyiko, kulitokea hali ya sintofahamu jinsi tiketi zilivyouzwa. Tulipata taarifa kuwa tiketi kutoka bodi zilifika tangu Oktoba 28, lakini tulipowaambia Mrefa juu ya kuweka alama katika tiketi wakasema hawajazipokea.”

Wakati huohuo, Kimebe amesema kuwa vurugu zilizotokea mara baada ya mchezo huo haziwahusu mashabiki wao na wanaostahili kulaumiwa na jeshi la polisi kwa kuwa walikubaliana baada ya mechi timu zisindikiwe na wanausalama lakini haikuwa hivyo.

Uongozi wa Prisons umepeleka malalamiko ya kuishitaki Mbeya City kutokana na kudai kuwa mashabiki wake waliwafanyia fujo na kuwajeruhi wachezaji wao kadhaa.


Katibu wa Prisons, Jumbe Sadick amesema: “Hivi sasa (jana) ninavyoongea kuna mashabiki sita wapo mahakamani wanasubiri hukumu kuhusiana na vurugu. Kuna wachezaji wetu walioumia Lugana Mang’amba, Ibrahim Mamba na Salum Kimanya ambao hawatacheza dhidi ya JKT Oljoro, Jumamosi (kesho).”

SOURCE: CHAMPIONI 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic