Kamwe hauwezi kusikia Manchester United wamefanya usajili kwa kuwa wamesikia Arsenal wamefanya hivyo, hali kadhalika kwa Arsenal.
Kila timu
inafanya mambo yake kwa kuangalia mipango yake kamili, kwamba inahitaji
wachezaji katika nafasi ipi na nini cha kufanya kwa ajili ya faida ya timu.
Benchi la
ufundi lina nafasi kubwa ya kuangalia wachezaji wa aina gani wahitajika wakati
msimu unapoanza na mzunguko wa kwanza unapomalizika kama sasa ilivyo kwa Ligi
Kuu Bara lazima kutakuwa na mabadiliko.
Benchi la
ufundi safari hii linakuwa na nafasi ya kutoa tena mapendekezo yake katika
mechi zilizobaki kuwa cha kufanya ni kitu gani na kama usajili wachezaji
wanaotakiwa ni wa aina na nafasi zipi.
Lakini hapa
nyumbani inaonekana mambo mengi yanakwenda tofauti na inawezekana mabenchi ya
ufundi hayana nguvu kubwa na badala yake usajili unaangalia zaidi mapendekezo
binafsi na hasa ya wanaotoa fedha.
Wako
wanaotoa fedha kwa ajili ya usajili katika klabu za Simba na YAnga, wanasikilizwa
kwa kuwa wanaonekana ni msaada mkubwa sana.
Wakati
mwingine wanafikia kusajili wachezaji ambao walikuwa hawahitajiki na benchi la
ufundi, halafu mwisho wanajikuta wakiingia katika kundi la kulazimisha wacheze
na kumpa kocha wakati mgumu.
Wanalazimisha
mchezaji waliomsajili acheze kwa kuwa wanaona walitumia fedha zao kwa ajili ya
kumsajili, lakini benchi la ufundi halikumhitaji, mwisho hapo unaanza ugomvi
kati ya watoa fedha na kocha, anaanzishiwa ‘zengwe’, kwamba uwezo wake mdogo.
Mifano iko
mingi kwa wachezaji kibao walio Yanga na Simba nah ii inatokana na ule usajili
wa kumrithisha mtu mmoja ambaye ana uwezo wa kutoa fedha za usajili au mshahara
kumlipa mchezaji fulani.
Pia
kumekuwa na tabia hizi klabu kuangalia upande mmoja imesajili wachezaji wangapi,
basi upande mwingine pia kutaka kujibu mapigo huku mambo yakionekana kwenda
kisiasa zaidi.
Angalia
mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Hussein Javu, anapoteza muda wake mwingi akiwa
benchi lakini juzi hapa Simba imesajili wachezaji huku kukiwa na taarifa
hayakuwa mapendekezo ya benchi la ufundi.
Dunia
inakwenda kasi sana katika suala la maendeleo, mambo yako tofauti kabisa katika
kipindi hiki. Viongozi wanaofanya usajili au wanaohusika na zoezi hilo
wanapaswa kukubali kujifunza na mwisho wabadilike.
Siasa au
ushabiki wa kutaka sifa, kama vile Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage
kusajili wachezaji subuleni kwake. Hiyo ni dalili ya mambo hayo
ninayoyazungumzia, ikifika wachezaji hao wamekwama basi ni tatizo.
Hivyo kuna
haja ya kugawanya mambo kitaalamu, yaani kama ni suala la kiufundi, basi
mafundi wapewe nafasi waifanye kazi yao badala ya watu wanaohusika na uongozi
au wenye fedha zao mfukoni kuingilia tu.
Tunakubaliana
na mgawanyo wa kazi kupitia vitengo, kamwe hakuna timu inayoweza kufanikiwa
bila mgawanyo wa kazi kama hivi, kipa, mabeki, viungo na washambuliaji. Halafu
baada ya hapo wote wanafanya kazi pamoja kupitia hiyo migawanyo.
Maana yake,
hata kwenye masuala ya uongozi pia kuna mgawanyo na baada ya hapo kila upande
unafanye kazi zake kwa juhudi kama timu ili kusaidia mafanikio ya pamoja
kupatikana. Kama itakuwa watu wengine wanajua kila kitu na wanadharau wengine
kwa kuwa hawana fedha au vyeo vya juu, basi mtakwama na kila siku mtatafuta
wachawi.
0 COMMENTS:
Post a Comment