SASA imekuwa ni kawaida kabisa kumsikia
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Yanga, Ibrahim Akilimali akilizungumzia jambo
fulani linaloihusu Yanga tena hadharani na mawazo au mazungumzo yake yakapewa
nafasi kubwa kabisa kwenye vyombo vya habari.
Akilimali ni kati ya wazee wanaoijua
Yanga, wameitumikia na ana mapenzi nayo makubwa sana, hilo halina ubishi na
ndiyo maana Wanayanga wengi, wanamheshimu sana.
Lazima kumpa heshima yake, ni kati ya
wapambanaji, amekuwa hataki mambo ya Yanga yaende shaghalabaghala, badala yake
anaona bora Yanga iendelee kuwa ileile ya mwaka 1947 na hajali kabisa kwamba
mabadiliko ya dunia, yanakwenda haraka sana.
Uongozi wa soka wakati wa akina
Akilimali, unapaswa kupongezwa maana ndiyo ulijenga angalau hata majengo katika
klabu hizo. Naamini mzee huyo hakuwa kiongozi lakini kati ya wanachama
wahamasishaji, ndiyo maana wazee wanaheshimiwa.
Pamoja na yote hayo, Yanga wana mambo
kadhaa wanalazimika kuwa makini la sivyo, Mzee Akilimali badala ya kuwa
mhamasishaji au mlinzi wa maslahi ya Yanga, anaweza kugeuka kuwa mbomoaji wa
klabu hiyo kwa kuwa tu amepewa nafasi kubwa afanye analotaka.
Sitaki kuingia kuingia kwenye katiba ya
Yanga na kuona nafasi anayopewa Mzee Akilimali kupingana na uongozi wa Yanga,
kulalama kila wakati au kusema chochote kama MC ni sahihi au basi tu ni heshima
kwa kuwa ni mzee na anapaswa kuheshimiwa!
Angalia mifano ya matukio ya hivi
karibuni, Mzee Akilimali aliwahi kumtimua aliyetaka kuajiriwa kama Katibu Mkuu,
Patrick Naggi. huyu jamaa alitokea Kenya, mimi pia nilimuunga mkono. Sababu ya
kumuunga mkono ni kwamba kweli klabu sasa zinahitaji makatibu wajuzi zaidi kama
ilivyoonekana kwa Naggi.
Lakini hakukuwa na sababu ya kutafuta
Mkenya, badala yake Mtanzania mwenye vitu kama alivyonavyo Nagi au angalau
anayemkaribia na ikiwezekana zaidi kwa kuwa Watanzania pia tunaweza kufanya
mambo yetu, si lazima sana wageni kila sehemu.
Baada ya hapo, naona kama Mzee Akilimali
kanogewa na sasa anasema lolote ili mradi tu, na wako wanaomuunga mkono kwa
kuwa wanayatupia macho matukio kwa jicho la kishabiki zaidi. Angalia Mzee
Akilimali alipoibuka na kusema hadharani kwamba Juma Kaseja hakutakiwa
kusajiliwa Yanga kwa kuwa eti alikosea na kuifungisha bao la tatu wakati
ikipambana na Simba na kulala kwa mabao 3-1 katika mechi ya kirafiki ya Nani
Mtani Jembe.
Tena akaulaumu uongozi kumsajili Kaseja
huku akisisitiza kwamba aliyetakiwa ni Ivo Mapunda aliyekwenda Simba, huku
akilaumu kwamba kumpa Kaseja Sh milioni 40 atue Jangwani lilikuwa ni kosa
kubwa! Kama haitoshi akaongeza aliandika barua kwa uongozi usimsajili Kaseja
akashangaa haikujibiwa.
Siku chache baadaye akaibuka tena na
kuutaka uongozi usimuache Kocha Fred Felix Minziro kwa kuwa wamekuwa naye
pamoja kwa kipindi chote pia ni Yanga damu! Kwangu naona Mzee Akilimali
anazungumza mambo mengi sana yasiyomhusu na wakati mwingine anakurupuka tu.
Mzee Akilimali ameanza kuvuka mipaka,
safari hii anazungumzia zaidi mambo ya ufundi ambayo hayamuhusu hata chembe na analazimika
kukubali kwamba kuna baadhi ya mambo ni vizuri angalau kujifunza, kujisomea, au
kuulizwa ukafundishwa au kuelezewa kabla ya kuyazungumzia.
Masuala ya Kaseja na Minziro ni ya
kiufundi, ingekuwa vizuri akaonyesha kuuamini uongozi wake na ikiwezekana kama
kuna jambo, basi yako anayoweza kuyasaidia kwa kuzungumza nao na kutoa maoni
yake na si kukimbilia kwenye “ma-ITV” au vyombo vingine vya habari.
Uhuru wa kutoa maoni kama mmoja wa wazee
wa Yanga anao, lakini asiutumie vibaya na kuanza kuingia kila sehemu.
Kumshambulia Kaseja bila ya kujali kwamba ni mwanajeshi wao aliye kazini si
sahihi. Yanga ina michezo mingi muhimu mbele yao ikiwemo ile migumu ya Ligi ya
Mabingwa Afrika, huo wa kirafiki umepita.
Kuamua uzuri wa Minziro pia si sahihi,
sina maana nataka Minziro afukuzwe, kama ni utashi wangu ningependa abaki kwa
kuwa ni mtu asiye na ‘kwere’ hata kidogo. Lakini suala hilo vema likaamuliwa na
watu wa ufundi wa Yanga ambao mara zote wamekuwa wakifanya kazi hiyo na si maneno
tu Mzee Akilimaliza!
Wakati umewadia, Mzee Akilimali
kuonyesha kweli ukongwe ni mali na azungumze kila jambo lakini baada ya
kutafakari kwanza. Apunguze kutanguliza ushabiki tu, sifa, kutaka kuonekana,
kuona raha kusikika na akumbuka huu ni mwaka 2013 unaokwenda ukingoni na si 1947.
Kheri ya mwaka mpya kwako Babu Akilimali.
FIN.
0 COMMENTS:
Post a Comment