Tabia ya kipa wa Simba, Ivo Mapunda kutundika taulo katika nyavu za
golini sasa inaelekea kufikia ukomo kwa kuwa licha ya waamuzi kadhaa kumkataza
kufanya hivyo wakati wa mechi, mwamuzi mwingine wa kimataifa ameliambia gazeti
hili kuwa ni marufuku kutundika taulo golini.
Ivo amekuwa na kawaida ya kutundika taulo kwenye nyavu kisha kuendelea
na mchezo, lakini kwenye Michuano ya Kombe la Chalenji, mwamuzi mmoja aliitoa
na kumtaka kuiweka chini na iwe nje ya goli, pia katika mechi ya Simba dhidi ya
Yanga, mwamuzi wa kati, Ramadhani Ibada wa Zanzibar alimkataza kuining’iniza
kwenye nyavu wakati mechi ikiendelea.
Mwamuzi Oden Mbaga amesema ni kosa kutundika taulo kwenye nyavu kwa
kuwa inaweza kuwachanganya wachezaji wakati wa mchezo.
“Kimsingi hairuhusiwi kabisa kuingia na taulo labda aliweke kwa nje
lakini siyo ndani ya lile goli tena siyo taulo tu bali na vitu vingine
vyovyote,” alisema Mbaga.
Wakati Ivo akiambiwa hivyo, makipa kadhaa wa Ulaya wamekuwa na kawaida
ya kutundika taulo kwenye nyavu na hawazuiliwi na waamuzi.
Wakati huohuo, Ivo amesema ana mpango wa kuchapisha taulo zitakazo
kuwa na nembo yake ili aweze kujiongezea kipato. "Fursa hiyo nimeona siku
nyingi. Nitakutana na kampuni mbalimbali kuona uwezekano huo," anasema
Mapunda.
Alisema hivi sasa taulo
anazotumia kujifuta jasho pindi anapokuwa uwanjani zina nembo mbalimbali lakini
atakoma kuzitumia pindi zenye nembo yake zitakapoanza kutoka.
0 COMMENTS:
Post a Comment