Timu ya JKT Oljoro inatarajiwa kwenda kucheza
mechi zake za kirafiki jijini Nairobi, Kenya, kwa ajili ya kujiandaa na
mzunguko wa pili wa ligi utakaoanza Januari, 25, mwakani.
Timu hiyo yenye maskani yake jijini Arusha,
itaumana na Machava FC ya Moshi inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza kabla ya
kutimkia Nairobi mnamo Desemba 24, mwaka huu kwenda kukipiga na timu za ligi
kuu ya huko.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Hemed Morocco, amesema
wanahitaji kucheza na timu za Kenya wakiamini kupata ushindani wanaouhitaji kwa
ajili ya maandalizi ya mzunguko wa pili.
"Tutacheza mechi zaidi ya tatu tukiwa
Nairobi na timu tofauti, bado hatujajua tutacheza na nani, kuna timu
tunaendelea kuzifuatilia kwa ajili ya mechi hizo ambazo tutazitaja muda si
mrefu.
"Tumechagua Nairobi kwa kuwa kuna ushindani
wa kutujenga kabla ya mzunguko wa pili kuanza, hata hivyo, tutakuja Dar es
Salaam pia tukisharudi Kenya kwa ajili ya mechi nyingine za mwisho, tutacheza
pia na timu za ligi kuu," alisema Morocco.








0 COMMENTS:
Post a Comment