Mshambuliaji mpya wa Yanga, Emmanuel
Okwi, kawaida anatumia jezi namba 25 na tayari anayeitumia katika kikosi hicho
ametakiwa kuachana nayo.
Okwi aliyekuwa tegemeo Simba, amejiunga
Yanga kwa kusaini mkataba wa miaka mwili na nusu na tayari Hati ya Uhamisho wa
Kimataifa (ITC) imetua TFF.
Taarifa tulizozipata
kutoka ndani ya kikosi hicho, zimesema mabosi wa Yanga tayari wameanza
mazungumzo na beki Ibrahim Job, ambaye huvaa jezi namba 25, ili amuachie Okwi
anayetarajiwa kutua leo jijini Dar akitokea kwao Uganda.
Mmoja wa viongozi wa timu hiyo amesema
Job amekubali kuiachia jezi hiyo kwa masharti kwamba anataka apewe jezi namba
13, hata hivyo imeonekana kuna ugumu kwa kuwa kuna taarifa jezi hiyo tayari
imeandaliwa maalum kwa nyota mpya wa kikosi hicho ambaye jina lake halijawekwa
wazi.
“Nimepata taarifa viongozi wamemfuata
Ibra (Job) wakimtaka aachane na jezi namba 25 ili aweze kupatiwa Okwi, ambaye
amekuwa akiitumia jezi hiyo tangu akiwa Simba,” alisema kiongozi huyo.
“Taarifa zilizopo ni kwamba Ibra
amekubali, lakini amewataka viongozi kumpatia jezi namba 13, lakini viongozi
wanasema atapewa mchezaji mpya ambaye hajajulikana. Hatujajua mwisho
utakuwaje,” kilisema chanzo chetu.
Kufuatia taarifa hizo, Championi
Jumatano lilimtafuta Job ambaye alikiri kuwepo kwa mpango huo huku akiomba
watafutwe viongozi wa klabu hiyo ndiyo watakaoweza kulitolea ufafanuzi zaidi
suala hilo.
Okwi aliondoka Simba kwenda kujiunga na
Etoile du Sahel baada ya kuuzwa ‘bure’ kwa Sh milioni 480,000, fedha ambazo
Simba hawajazipata hadi leo, hali hiyo imesababisha kuamsha machungu kwa
wanachama na mashabiki wa Simba.








0 COMMENTS:
Post a Comment