Beki wa kimataifa wa Simba, Joseph Owino amemtaka Mganda mwenzake
aliyesajiliwa na Yanga hivi karibuni, Emmanuel Okwi kuachana na vitendo vya
starehe ili aweze kuwa katika kiwango kizuri kwa muda wote atakaokuwa na klabu
hiyo kwa kuwa hiyo ndiyo siri pekee ya mafanikio yake.
Owino amesema kuwa endapo Okwi hatafanya hivyo, itakuwa ni vigumu
kwake kufikia mafanikio aliyoyapata awali wakati akiwa Simba.
Alisema anaifahamu vilivyo tabia ya Okwi kuwa ni mtu wa mambo mengi
tangu walipokuwa pamoja SC Villa Uganda na baadaye Simba, ambapo amesisitiza
kuwa huu ndiyo muda wa mabadiliko ili afanye kazi na hakuna siri ya ziada ya
mafanikio zaidi ya hiyo.
"Kama asipokuwa makini na kuendekeza starehe, mambo yanaweza
yakamwendea vibaya na kujikuta asifikie kiwango chake kama alichokuwanacho
wakati ule akiwa Villa na baadaye Simba.
"Namjua vizuri sana Okwi, kuwa ni mtu wa mambo mengi lakini
anatakiwa kupunguza mambo hayo kwa faida ya soka lake lakini pia asichukiwe na
mashabiki wa timu yake mpya ya Yanga," alisema Owino.
Okwi ametua Yanga akitokea SC Villa ya Uganda kwa mkataba wa miaka
miwili na nusu na tayari ameanza kuonyesha makali baada ya kuifungia bao timu
hiyo katika mechi dhidi ya Simba, Jumamosi iliyopita katika mechi ya Nani Mtani
Jembe, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.







0 COMMENTS:
Post a Comment