Kocha Mkuu wa Azam FC, Joseph Omog, ameomba
mechi tano za kirafiki kabla ya michuano ya Kombe la Mapinduzi kuanza mnamo
Januari 2, mwakani.
Kocha huyo aliyesaini kuifundisha Azam
hivi karibuni akichukua nafasi ya Muingereza, Stewart Hall, anataka mechi hizo
kwa lengo la kuona viwango vya wachezaji wake na kuteua kikosi cha kwanza.
Katibu Mkuu wa Azam FC, Idrissa Nassoro, alisema kocha wao ameomba mechi tano
za kirafiki na wana imani kuwa zitaisaidia Azam kutetea Kombe la Mapinduzi.
“Kocha Omog ametaka mechi tano za
kirafiki kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Mapinduzi ili kukitayarisha
kikosi chake na kufanikiwa kutetea kombe letu.
“Kocha amekuja na falsafa mpya ambapo
anahitaji kukibadilisha kikosi ili kiweze kuwa imara hadi kwenye ligi kwa
kuhakikisha tunamaliza katika nafasi nzuri.
“Lengo letu ni kuona tunafanikiwa
kutetea Kombe la Mapinduzi, ndiyo maana tunajiandaa vya kutosha kuhakikisha
tunafanikisha lengo letu,” alisema Nassoro.
Kocha huyo alitarajiwa kutua Ijumaa
iliyopita kwa ajili ya kuanza rasmi kazi ya kukinoa kikosi cha Azam ambacho
kwenye Ligi Kuu Bara kipo katika nafasi ya pili kikiwa na pointi 27.
0 COMMENTS:
Post a Comment