JUMAMOSI iliyopita, mabingwa wa
Tanzania, Yanga walipoteza mchezo wao wa kirafiki wa Nani Mtani Jembe dhidi ya
watani wao Simba baada ya kukutana na kipigo cha mabao 3-1.
Katika mechi hiyo, mashabiki wengi zaidi
wa Yanga walijitokeza wakiamini timu yao itaibuka na ushindi kwa kuwa ina
kikosi bora kabisa katika kila idara.
Kuongezeka kwa Emmanuel Okwi katika
kikosi cha Yanga, kulisababisha kuonekana kama mchezo huo wa watani tayari
matokeo yalipatikana na uhakika ulikuwa ni Yanga kuibuka na ushindi.
Ndiyo maana wiki moja kabla ya mchezo
huo, mashabiki wa Yanga walikuwa wakitamba barabarani kwamba wanachotaka kujua
ni idadi ya mabao watakayowafunga watani wao lakini suala la ushindi lilikuwa
na uhakika tayari!
Ajabu Yanga wanaonyesha ni wasahaulifu
sana, si zaidi ya miezi miwili tokea Simba walipowaamsha kwa kusawazisha mabao
yote matatu waliyofunga katika kipindi cha kwanza na kufanya matokeo ya mechi
hiyo ya Ligi Kuu Bara kumalizika kwa sare ya bao 3-3 wakati Yanga waliamini
ilikuwa ni siku sahihi ya kulipa kisasi cha mabao 5-0.
Soka ina mambo yake, kila mechi haishi
bila kuacha gumzo ndiyo maana Yanga ikajisahau tena na safari hii ikakutana na
kipigo cha mabao 3-1 na Simba wakaweka rekodi ya kwanza kuishinda Yanga ikiwa
chini ya uenyekiti wa Yusuf Manji.
Kufungwa kwa Yanga kwa idadi hiyo ya
mabao ilionekana kama ajabu kwa mashabiki lakini kama ilivyo ada, lazima kuwe
na wa kubebeshwa lawama, mashabiki ‘wakamuangukia’ kipa Juma Kaseja.
Kaseja alifungisha bao la tatu kwa
bahati mbaya, alianguka wakati akijaribu kuumiliki mpira na Awadhi Juma wa
Simba akamchepuka na kuupachika mpira wavuni.
Baada ya hapo gumzo likawa ni Kaseja
ndiye msaliti na wengine wakisema ametokea Simba. Ajabu zaidi hata mmoja wa
wazee wa Yanga, ….Akilimali naye akathubutu kusema uongozi wa Yanga ulikosea
kumsajili Kaseja kwa kuwa ni Simba na badala yake ungemsajili kipa Ivo Mapunda.
Kitu ambacho ni cha kuzungumzia hapa ni
ujasiri wa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Mehbub Manji ambaye siku moja tu baada ya
Yanga kufungwa mabao 3-1, aliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kufafanua
mambo kadhaa.
Moja ya mambo hayo, Manji alieleza kosa
la Kaseja ni sehemu tu ya mchezo na kuwataka mashabiki kuachana na kumlaumu na
badala yake waungane na kuangalia watarekebisha vipi makosa yaliyojitokeza ili
waweze kwenda mbele.
Lakini Manji pia alimkemea hadharani
Mzee Akilimali kwamba alichosema hakikuwa sahihi na hapaswi kumshambulia Kaseja
au kuonyesha uongozi ulikosea kumsajili kama amavyo alisema yeye.
Manji ameonyesha ujasiri na tofauti
kubwa na viongozi wengi waliopita wa Yanga na hata Simba, kwani kamwe hawawezi
kuwasaidia wachezaji wao wanapokuwa katika wakati mgumu kama ilivyokuwa kwa
Kaseja.
Manji hawezi kumtetea Kaseja huku akijua
amefanya madudu, ameonyesha ni mwelewa lakini anayetambua kuwa kwenye soka,
makosa ni lazima na Kaseja ni mmoja wa makipa bora Afrika Mashariki na Kati
ambaye angefurahi kuona Yanga inashinda ili kuthibitisha uwezo wake.
Kumshambulia kwa kujali maneno ya
kishabiki zaidi haikuwa sahihi, Manji ameonyesha si mwoga na ameweka mambo
hadharani na leo anaeleweka na wengi. Lakini viongozi wengi wamekuwa kimya na
hata wakati mwingine kuungana na wengine kuwashambulia wachezaji.
Manji amefungua njia, suala la Kaseja ni
moja tu. Katika klabu za soka nchini kuna mambo mengi na kama wenyeviti na
viongozi wengine wataamua kuwa wakweli, wasioyumba au kufanya kazi zao kinafiki
kama ilivyokuwa kwa mwenyekiti huyo wa Yanga basi mambo yatabadilika.
0 COMMENTS:
Post a Comment