December 24, 2013




Kazi anayotakiwa kufanya kocha wa timu imeonekana wakati wa mechi ya watani, Simba na Yanga walipovaana katika kipute cha Nani Mtani Jembe.
 
Kocha Mkuu wa Simba, Zradvko Logarusic, alionyesha ni anayejiamini, anayeweza kufanya uamuzi mara moja bila ya kuchelewa na kweli timu yake ikashinda.

Katika mechi ya juzi kwa kuwa ilikuwa ni kama ya kirafiki, kila timu ilipewa nafasi ya kubadili wachezaji sita, Logarusic akawaonyesha wachezaji wa Simba kwamba katika kikosi chake, hakuna staa zaidi yake.
Kocha huyo raia wa Croatia alifanya mabadiliko yote sita, lakini burudani kubwa ilikuwa ni namna alivyowabadilisha wachezaji hao bila ya kupoteza muda hata kidogo, hata kama kosa lingeonekana ni dogo kwa mashabiki.
Kweli hataki mchezo kwa kuwa mabadiliko yake ya kwanza yalianza katika dakika ya 26 alipomtoa Said Ndemla ambaye alichezeshwa namba 10 iliyoonyesha kumshinda, nafasi yake mara moja ikachukuliwa na Ramadhani Singano ‘Messi’ ambaye aling’ara vilivyo.
Dakika tano baadaye, Logarusic akamuita mkongwe Henry Joseph kwenye benchi, kisa? Alikosea pasi moja tu ambayo ilionyesha hayuko makini, akapumzishwa na nafasi yake akachukua Ramadhani Chombo ‘Redondo’.
Hiyo ni rekodi mpya kwa kocha kufanya mabadiliko ya wachezaji wawili katika mechi ya watani Yanga na Simba na huenda kama angepoteza mchezo basi angekuwa kwenye lawama kubwa. Yeye mwenyewe anasema hajali presha badala yake ni kazi.
“Nilijua lolote linaweza kutokea lakini huo ni ujumbe kwa wachezaji wangu kwamba nataka wafuate maelekezo yangu bila ya visingizio,” anasema Logarusic.
Kweli alionyesha hajali kwani kipindi cha pili alifanya mabadiliko mengine manne, akianza na dakika ya 56, yaani dakika 11 tu baada ya kuanza kipindi cha pili, akamtoa Haruna Chanongo baada ya kutoa pasi kizembe, akaingia Uhuru Selemani.
Dakika mbili baadaye akampumzisha Amissi Tambwe ambaye alikuwa amefunga mabao mawili ambapo Simba ilikuwa inaongoza wakati huo, nafasi yake ikachukuliwa na Amri Kiemba.
Dakika ya 73, akamtoa Awadhi Juma aliyekuwa ameumia na kumuingiza Zahoro Pazi na baadaye dakika ya 84 akamtoa Chombo aliyeingia kuchukua nafasi ya Henry na kumuingiza Abdulhalim Humud kuongeza ulinzi ili kulinda mabao.
Inawezekana mabadiliko hayo yalitokana na kocha huyo kuwa na nafasi ya kubadilisha watu sita, lakini hata ingekuwa watatu tu, bado ni sehemu ya kuonyesha kocha anapaswa kujiamini kiasi gani, kuwa na uamuzi wa haraka na kujiamini.
“Mimi ndiyo kocha, naona kipi sahihi katika wakati upi. Naweza kufanya mabadiliko na kitu kisiwe kizuri, lakini bado natakiwa kufanya kazi si kwa kuangalia hisia za mashabiki au viongozi na kila mmoja ajue kila ninachoamua ni kwa ajili ya kitu kizuri cha timu, si mimi binafsi,” anasema Logarusic akionyesha kujiamini.
Siku mbili kabla ya mechi, Logarusic aliwaondoa wachezaji wengine kwenye kambi wakiwemo nyota kama Gilbert Kaze na Betram Mwombeki. Wengi waliona ajabu lakini mwisho ametimiza alichotaka na kujenga kuaminiwa.
Championi lilikuwa la kwanza kukataa kocha mpya wa Simba hakuwa yule aliyetangazwa mwanzo, lakini likamuelezea Logarusic na misimamo yake, sifa yake kwa mashabiki wa Gor Mahia ya Kenya, namna wanavyomthamini na kufikia kusema ubingwa wao walioupata chini ya kocha Bobby Williamson, Logarusic ndiye anastahili kwa kuwa alijenga timu.
Sifa zake ni ujeuri lakini ameonyesha ni wenye manufaa na makocha wanatakiwa kuwa wenye uwezo wa kuamua na wakikosea wakubali makosa.

1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic