Selemani Matola ataonja utamu wa kuwa
Kocha Mkuu Simba kwa zaidi ya saa 96 baada mwenye nafasi hiyo kuridhia
aitumikie.
Kocha Mkuu, Zdravko Logarusic,
amekubali Matola apewe nafasi hiyo kuanzia leo Jumatatu hadi Ijumaa asubuhi
atakapowasili akitokea kwao Croatia.
Chanzo kimesema hali hiyo inatokana na
Logarusic kuchelewa kurejea nchini.
“Kweli kocha katuambia atachelewa na
nafasi ya ukocha mkuu apewa Matola hadi hapo atakaporudi na ametaka tumwamini,”
kilisema chanzo.
Championi Jumatatu lilimtafuta
Logarusic kutoka kwao Croatia ambako yuko mapumzikoni, naye alisema amepitisha
hilo lakini amekuwa akiwasiliana na Matola.
“Yeye atachukua nafasi yangu kwa muda,
ninamwamini katika siku chache tulizofanya naye kazi.
“Tulipanga kila kitu kabla ya kuondoka,
anajua nini kifanyike na sasa anajua nini ninachotaka,” alisema Logarusic
aliyeingia mkataba wa miezi sita kuinoa Simba.
Kocha huyo wa zamani wa Gor Mahia ya
Kenya aliendelea kusema: “Kuhusiana na programu, tayari kila kitu anacho Matola
kama tulivyokubaliana.
“Kama nilivyosema ninamwamini na
ninajua ataanza vizuri katika mechi ya kwanza ya Kombe la Mapinduzi.”
Kuhusiana na hilo, jana Matola alisema:
“Nimepokea kwa mikono miwili, ingawa itakuwa ni muda mchache lakini najisikia
faraja kuwa kocha mkuu hata kama ni kwa muda.
“Najua ni mzigo mzito kwa kuwa Simba ni
kubwa, lakini nakuhakikishieni utabebeka tu na kocha akirudi atakuta
tunaendelea vizuri.”
Kabla ya kuondoka, Logarusic alifanya
kikao na Matola, wakapanga programu kwa ajili ya michuano hiyo.
Matola ataanza kuiongoza timu hiyo katika
mechi ya ufunguzi ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya AFC Leopards ya Kenya
itakayochezwa keshokutwa Jumatano.
Matola ameonekana kuelewana vizuri na
Logarusic, siku chache baada ya kupandishwa kutoka timu ya vijana baada ya
benchi la ufundi lililokuwa chini ya Abdallah Kibadeni na msaidizi wake,
Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ kufutwa kazi.
0 COMMENTS:
Post a Comment