Na Saleh Ally
KUZAGAA kwa taarifa za kufariki dunia kwa Mzee Small kuliwachanganya
watu wengi sana, lakini bado ilionekana hakuna uhakika katika suala hilo.
Taarifa za kifo chake zilianza kuzagaa Jumanne, saa 4 usiku na
ilielezwa amefariki muda mchache uliopita na msiba ulikuwa nyumbani kwake
Tabata jijini Dar es Salaam.
Kadiri muda ulivyokuwa unasonga mbele, taarifa za kifo cha Mzee Small
ziliendelea kuenea kwa kasi kubwa huku kwenye mitandao ya kijamii zikipata
nafasi kubwa.
Achana na blogu mbalimbali kuanza kuandika kuhusiana na ‘kifo’ hicho,
kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook, Instagram na Twitter, watu mbalimbali
wakiwemo wasanii maarufu walikuwa wakiweka picha zake na kumuombea apumzike kwa
amani (R.I.P).
Gazeti hili mara moja lilianza kufuatilia kutaka kujua kuhusiana na
ukweli, mafanikio ya kwanza yalikuwa ni kuzungumza na mwanaye aitwaye Yunus,
ingawa alikuwa amelala, aliamka na kupokea simu ya Championi na kusema mzee
wake ni mzima.
Lakini gazeti hili harikudhika, juhudi zikafanyika hadi kumpata mkewe,
Mama Said ambaye alithibitisha kwamba mumewe, Said Ngamba au Mzee Small ni
mzima na alikuwa amelala.
“Lakini unaweza usiamini, ngoja basi nimuamshe ili upate uhakika,”
alisema na kusikika akimuita, “Mzee Small, Mzee Small, zungumza na huyu ndugu
yako.”
“Mzee Small hapa, mimi ni mzima. Taarifa ulizosikia si sahihi,”
alisema Mzee Small mara baada ya kuichukua simu.
Baadaye akasikika tena Mama Said akisema: “Nafikiri umemsikia baba,
basi tumuache apumzike.”
Ushirikiano huo wa Mama Said ulitoa hofu ya taarifa hizo za kifo
zilizokuwa zikienezwa huku haijulikani yupi aliyekuwa ameamua kufanya hivyo na
kusambaza taarifa zisizokuwa na uhakika.
Juzi mchana, timu ya Championi ilifika nyumbani kwa Mzee Small eneo la
Tabata kumtembelea, kubadilishana naye mawazo, kumpa pole na kutoa mchango
kidogo kumsaidia matibabu (si lazima kusema kiasi gani).
Baada ya kufika Tabata, timu ya gazeti hili ikiongozwa na Mhariri
Kiongozi, Mhariri wa Championi Jumatano, Phillip Nkini na waandishi wawili,
Khatimu Naheka na Hans Mloli, ilipewa taarifa Mzee Small alikuwa amekwenda
mazoezini.
Mipango ya kumfuata ilianza, lakini ghafla Mzee Small aliwasili akiwa
katika pikipiki na kupokelewa na baadhi ya majirani zake ambao amekuwa akiwatania
ni wachumba zake.
Mzee Small alisaidiwa kushuka kwenye pikipiki na baada ya hapo
akaambiwa kuna wageni wake kutoka Championi. Aliwapokea na mazungumzo yakaanza
kabla ya yeye kuomba akapunguze nywele zake.
“Mke wangu amekuwa akiniambia kwamba hizi nywele si nzuri, zimekaa
vibaya. Si unaona, nafikiri tungekwenda nikapunguze kidogo halafu wote
tutakwenda nyumbani,” alisema na wote wakakubali.
Kwa kinyozi hapakuwa mbali, Mzee Small aliingia pamoja na timu nzima
ya Championi, wakati wakinyoa mazungumzo yalianza na akaanza kusimulia mkasa
huo wa kuzushiwa kifo akiuita ni bomu.
“Hili bomu la leo la kuzushiwa kifo limeniweka katika wakati mgumu,
watu wamekuwa wakipiga simu mfululizo wanataka kujua kama ni hai au la.
“Nimeshangazwa sana, nilitaka kujua huyo aliyezusha hayo yote ni nani,
lakini naweza kusema nawashukuru hao waliozusha maana wamenionyesha kitu kimoja
ambacho sikutegemea.
“Mapenzi ya watu kwangu, kweli watu wengi wamenipigia sana wakitaka
kujua kama ni kweli au la, naendeleaje na kwa nini imekuwa hivyo. Hadi sasa
simu zinaendelea kuingia, kumbe kuna Watanzania wanaonijali.
“Hakika maisha ni magumu, nateseka lakini angalau nina nafuu na kila
siku, mara mbili, asubuhi na jioni natakiwa kufanya mazoezi,” anasema Mzee
Small.
ENDELEA kusoma kuhusiana na Mzee Small, hali yake ya kuumwa, namna
anavyoendesha maisha, anavyomzungumzia mkewe huku akitangaza vita na yoyote
atakayemgusa.
USIKOSE JUMATATU.
SOURCE: CHAMPIONI







0 COMMENTS:
Post a Comment