Na Saleh
Ally
EMMANUEL
Arnold Okwi amesaini mkataba wa miaka miwili na nusu kuichezea Yanga, upande wa
Simba wanapinga suala hilo, bado hakijaeleweka vizuri.
Wakati
Simba wanapinga, tayari Uhamisho wa Kimataifa (ITC) umetua nchini na Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF) linasubiri kidogo tu, halafu litatangaza uhalali wa Okwi
kuruhusiwa kuichezea Yanga au la!
Kwa msimu
wa pili mfululizo, Simba imeonekana ni ya kupoteza vizuri dhidi ya Yanga na
tayari timu hiyo ya Jangwani imesajili wachezaji watatu nyota kutoka Simba
ambao walikuwa mahiri na msaada mkubwa kuunda kikosi bora cha Msimbazi.
Okwi,
Kelvin Yondani, Mustapha Ally ‘Barthez’ ambaye hayuko kikosi cha kwanza na Juma
Kaseja, lakini Simba pia imempoteza kiungo wake bora, Haruna Moshi ‘Boban’,
katika mazingira yaliyoonyesha hakukuwa na umakini mkubwa.
Inawezekana
Boban alikuwa ana matatizo, lakini hakuna kiongozi wa Simba aliyethubutu
kuzungumza hadharani zaidi ya kulalama chinichini, sasa safu ya kiungo inayumba
na baadaye ikawa upande wa kipa na viungo wa pembeni.
Kibiashara,
timu huwauza wachezaji wake bora si kuwaachia tu! Leo Arsenal haiwezi kumuachia
Theo Walcott kizembe, au Man United ikamuacha Wayne Rooney aende eti ni mtovu
wa nidhamu au ameshuka kiwango, lazima ipate faida. Lakini Simba inaendelea tu
kutoa sadaka! Maana haijapata hata senti.
Yanga
wameonyesha wanaelewa umakini wa wachezaji bora na muhimu, wakati Simba
walikubali Okwi aondoke bure ikiwa katika kipindi kigumu cha michuano ya Ligi
ya Mabingwa Ulaya, Yanga wamemsajili katika kipindi kama hicho kwa kuwa
wanahitaji huduma yake.
Jangwani
wanatambua mchango wa Okwi katika michuano ya kimataifa, alionyesha hayo Simba
ilipocheza na timu za Algeria na Sudan katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kukosekana kwake dhidi ya Libolo ya Angola, Simba ikawa nyanya na kunyanyaswa.
Yanga wana
hesabu nyingi za msingi kuliko Simba? Au Simba wanapuuzia sana mambo kutokana
na kutojali? Angalia Yondani, Kaseja na sasa Okwi, hawaoni matunda yao
yanakwenda bila faida kusaidia upande mwingine?
Yondani:
Wakati
Yanga inaanza mipango ya kumchukua, Simba walikuwa wamelala na mchezaji alisusa
kwa madai ya kutoelewana na viongozi, akakimbilia kwao Mwanza na kujificha,
hakuna kiongozi aliyejali sana.
Lakini siku
Yanga walipofanikiwa kumchukua, Simba wakacharuka na kuanza kudai mambo kadhaa
huku wakionyesha Yanga walikuwa ni tatizo.
Mwisho
wakashindwa, Yondani akatua Yanga na sasa ni tegemeo katika safu ya ulinzi ya
timu hiyo. Kuthibitisha kweli Simba ilipoteza mchezaji bora, ameipa Yanga
ubingwa na juzi ameteuliwa kuwa nahodha wa Kilimanjaro Stars.
Kaseja:
Hata kama
kuna unazi, lakini hakuna asiyejua Kaseja ni kipa bora hapa nchini. Simba
walimuacha akiwa nahodha wa kikosi chao, nahodha wa timu ya taifa, Taifa Stars,
na kipa namba moja nchini.
Simba
wakasema kiwango chake kimeshuka, lakini zilikuwa siasa tu za kutaka Abel
Dhaira apate nafasi ya kudaka, hivyo Kaseja alilazimishwa kuondoka Simba.
Ajabu,
Dhaira kadaka nusu msimu, Simba wamesema ameisha, wamemuacha na kusajili makipa
wawili kwa gharama nyingine tofauti.
Lakini
awali walianza juhudi za kumshawishi Kaseja kurudi, wakawa wamechelewa na Yanga
wakawahi, hili pigo lingine.
Barthez:
Alikuwa
kipa namba mbili wakati Simba inaichakaza Yanga kwa mabao 5-0, alikuwa kwenye
benchi. Yanga ikamsajili bure, Simba haikujali muda wote iliopoteza kumkuza,
kitu ambacho timu zinazojua biashara haziwezi kukubali hata kidogo, akaipa
Yanga ubingwa wa Kagame.
Okwi:
Blaah,
blaah nyingi kuhusu suala hilo, zilikuwa zinatafuta ukingo, sasa wakati
umewadia, Okwi amejiunga na Yanga kwa bei chee na siku mbili hizi, Simba
wamekuwa wakihaha kuzuia.
Bado hakuna
uhakika, inawezekana wakashinda au kushindwa katika hili, lakini mwisho Yanga
wameonyesha nia na wepesi wa kutambua ubora.
Kitu kizuri
kwa wakati mwafaka, tofauti na Simba ambayo vitu vikiwa vizuri inavihofia. Kila
anayekuwa maarufu anakuwa matatizo kwa kuwa viongozi wake wanataka wachezaji
waoga au wasiojitambua watakaoelekezwa kila wanachotaka.
Wakati
Etoile du Sahel ilionyesha haitalipa fedha hizo ni pale ilipowaambia Simba
inataka kumrudisha Okwi, wao wakakataa, tayari jibu lilipatikana.
Lakini leo
mchezaji huyo ambaye alilipwa dola 40,000 kuongeza mkataba Simba siku chache
kabla ya kujiunga na Etoile, akapokea dola 45,000 za Etoile akisubiri ziada,
sasa amelipwa dola 50,000 kujiunga Yanga.
Zaidi ya Sh
milioni 200 mkononi mwa Okwi katika kipindi cha msimu mmoja, Simba imepata
hasara ya zaidi ya dola 60,000 (fedha za kumuongeza Okwi mkataba, zile
zilizotumika kama tiketi na matumizi ya kushughulikia malipo ya Okwi. Kama
haitoshi, dola 300,000 (Sh milioni 480) zinaendelea kuwa hadithi!
Wachezaji
hao watatu ni wale waliokuwa katika kikosi kilichoifunga Yanga mabao 5-0, maana
yake Yanga wameangalia ubora na kuwachukua wote.
Kitu
kingine, kati ya hao watatu, wawili walifunga mabao matatu katika ile mechi.
Okwi alifunga mawili na Kaseja moja kwa penalti.
Lakini
Yondani, Kaseja na Okwi wote ni wachezaji wa timu za taifa pia wa kiwango cha
juu, ondoka yao Simba inaonyesha kuwa hakuna mipango wala hesabu sahihi za
kulinda vilivyo bora.
Lakini kama
Okwi ataichezea Yanga, maana yake Simba haikuwa kibiashara, hakuna mipango
sahihi na viongozi wake wamelala!
FIN.








0 COMMENTS:
Post a Comment