JUZI Jumatatu, Mzee Small alikuwa
akielezea kuhusiana na namna ambavyo ndugu zake walielekeza lawama kwa mkewe,
Mama Said kwamba ni mtu mbaya, yeye akapinga na kutaka waachane na mawazo
potofu kwa kuwa amekuwa akijitolea sana hasa katika kipindi hiki kigumu kwake.
Lakini pamoja na hivyo, Mzee Small
anaeleza kwamba katika matibabu yake amepita kila sehemu. Wakati fulani aliwahi
kumchukua mganga kutoka Kigoma na alipofika Dar es Salaam akamtimua.
Sababu za kumtimua ni zipi, maana
itakuwa kitu cha ajabu wakati mwigizaji huyo mkongwe anataka kupona kutokana na
kukabiliwa na ugonjwa wa kupooza upande mmoja wa mwili wake ? Endelea.
SUALA la kuumwa linaonyesha kurudisha
nyuma mambo mengi sana ya Mzee Small hasa kuhusiana na maisha yake ya kila
siku.
Katika kipindi hiki, Mzee Small amekuwa
hana uwezo tena wa kufanya kazi zake za sanaa na muda mwingi anautumia
kupambana na kujiuguza ili arudi katika maisha yake ya zamani.
Mzee Small ni maarufu katika eneo
analoishi la Tabata na jirani zake wengi wanaonyesha mapenzi makubwa kwake kwa
kuwa ameishi nao vizuri.
Kabla ya kuanza kuugua, kazi kubwa
aliyokuwa akifanya ni sanaa lakini pamoja na hivyo amekuwa na mradi wake wa
visima vya maji.
Wakazi wa eneo hilo kwa asilimia kubwa
wamekuwa wakichota maji kwenye visima vinavyomilikiwa na Mzee Small na kipindi
hiki anashindwa kufanya kazi hiyo kwa ufasaha.
Akirudi kuelezea kuhusiana na ugonjwa wake
namna ambavyo umekuwa ukimweka katika wakati mgumu, Mzee Small anasema aliwahi
kumuita mganga wa kienyeji kutoka mkoani Kigoma.
“Kabla ya mganga huyo kuja hapa Dar es
Salaam, alitaka nimuandalie sehemu ya kulala. Basi nilifanya hivyo kwa kuwa
nilikuwa nahitaji tiba,” anasema Mzee Small.
“Kweli mganga alikuja na akakuta
nimemuandalia chumba, akanieleza alikuwa na uwezo wa kunitibu hadi nipone na
akasema alikuwa anataka kulipwa shilingi laki tatu kwa huduma yote.
“Fedha hizo ni nyingi sana, lakini
sikuwa na ujanja nikakubali na kumueleza nitamlipa, aanze tu kazi maana
nilikuwa natamani sana kupona ili nirudi katika maisha yangu ya kawaida.
“Yule mganga akaanza tiba, kweli alikuwa
akinichua lakini ajabu wakati anafanya kazi ya kunichua maumivu yalikuwa makali
sana upande ambao ni mzima.
“Maumivu hayo ya upande uliokuwa mzima
yalikuwa makali sana kuliko hata upande uliokuwa na matatizo, nikajaribu
kumkumbusha mganga kwamba upande uliokuwa na matatizo ulikuwa si ule aliokuwa
akiutibu.
“Lakini hakuwa anaelewa, aliendelea tu
kunichua upande ambao haukuwa na matatizo huku akisisitiza kwamba upande huo
ndiyo ulikuwa wenye matatizo.
“Kweli nilikuwa nataka kupona, lakini
nilishindwa kuvumilia. Nilimueleza Mama Said (mkewe) kwamba nimeshindwa, maana
maumivu yalikuwa makai utafikiri ananikata visu, nilishindwa.
“Siku moja akiwa ananichua, kawaida
nilikuwa nalala hapa (anaonyesha kibarazani kwake), nikamuambia nimechoka na
tiba hiyo maana naona ilikuwa inazidi kunipatia maumivu tu.
“Nikaamua kumfukuzia mbali, wakati
ananichua nikamuambia Mama Said aingie ndani na kuleta fedha yake aliyokuwa
ananidai, nikamlipa.
“Alionekana kama alikuwa hajanielewa,
lakini nilimsisitiza kwamba hayo ndiyo yalikuwa malipo yake kama
tulivyokubaliana. Hata kama nilikuwa sijapona, basi mara moja aondoke zake.
“Ilionekana kama haamini vile, alianza
kuhoji sababu za kumfukuza wakati alikuwa akinitibu. Nikaona haelewi vizuri,
nikaomba panga langu na kumtaka aondoke mara moja.”
MZEE SMALL amecharuka, amebeba panga
lake na kumtaka mganga wa kienyeji kutoka Kigoma aondoke mara moja katika eneo
lake la nyumbani. Lakini inaonekana kama mganga bado haelewi kinachoendelea.
Je, nini kitafuatia?FUATILIA ZAIDI KESHOKUTWA IJUMAA.
SOURCE: CHAMPIONI







0 COMMENTS:
Post a Comment