Msafara wa watu 29 wa timu ya taifa ya
vijana ya wanawake, The Tanzanite, leo saa nne asubuhi unatarajiwa kuelekea
nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kwenda kurudiana na timu ya vijana ya nchi
hiyo katika mchezo utakaopigwa Jumamosi ijayo.
Katika mchezo wa kwanza wa raundi ya
pili kufuzu Kombe la Dunia la Wanawake kwa Vijana, Tanzanite walifungwa mabao
4-1. Mechi ilichezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, takribani wiki mbili
zilizopita.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, jana,
Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura,
alisema katika msafara huo, wachezaji wanatarajiwa kuwa 24 na benchi la ufundi
la watu watano na wataondoka na Fast Jet.
“Jumla ya watu 29 wanatarajiwa kusafiri
kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya timu ya soka
ya wanawake ya vijana wa nchi hiyo,” alisema Wambura.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Rogasian
Kaijage, alisema kuwa wamejiandaa vya kutosha kuhakikisha wanarejea na ushindi
katika mchezo huo wa marudiano, licha ya mechi ya kwanza kufungwa.
The Tanzanite inahitaji ushindi wa mabao
4-0 au zaidi ili isonge katika hatua inayofuata.
Katika hatua nyingine, Wambura alisema
wameongeza magari ya kutosha ya wagonjwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam wakati Simba na Yanga zikivaana katika mechi ya Nani Mtani Jembe
itakayochezwa Jumamosi.
0 COMMENTS:
Post a Comment