Kwa muda wa miezi kadhaa SALEHJEMBE
imekuwa ikitoa makala mbalimbali zikielezea na kuonyesha mazingira ya viwanja
vinavyotumika katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Wakati fulani ilifikia hadi Bodi ya
Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) kutangaza kuvifungia baadhi ya viwanja hivyo. TFF
imeeleza sababu mbalimbali na kuwataka wahusika wafanye marekebisho
yanayotakiwa, la sivyo timu zinazotumia viwanja vilivyofungiwa zitalazimika
kutovitumia.
Lakini inawezekana TBL ilipitiwa na
kuusahau Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi ulisahaulika, maana hauna hadhi ya
kuchezewa Ligi Kuu Bara.
Swali, TPL walihofia kwa kuwa
unatumiwa na timu za jeshi, au walipitiwa tu?
Uwanja wa Mabatini uliopo Mlandizi Pwani nao unatumiwa katika
baadhi ya mechi kwenye ligi hiyo, ukiwa ni uwanja wa nyumbani wa Ruvu Shootings,
lakini haumo kwenye orodha ya vile vilivyofungiwa.
| BENCHI LA KAGERA |
Uwanja huo upo umbali wa kilometa moja
kutoka kituo cha daladala cha Mlandizi. Maji ya kumwagilia yapo na hiyo
imesababisha sehemu ya kuchezea kuwa na ubora mzuri kwa kuwa nyasi ni nyingi na
zinavutia.
Pamoja na uzuri huo wa sehemu ya
kuchezea, sehemu ya majukwaa haina ubora mzuri na kuna sehemu ambazo
zinaonyesha wazi hazijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu.
Kuna jukwaa ambalo limegeuzwa kuwa
sehemu ya kujisaidia, wakati wa mechi kuna wachezaji na mashabiki ambao
wamekuwa wakisimama hapo kisha kujisaidia haja zao na wengine kuoga kabisa.
Uzio uliozunguka uwanjani hapo nao pia
ni kama wa kuunga-unga, matundu ni mengi na endapo kunatokea purukushani basi
madhara yanaweza kuwa makubwa zaidi.
Siku ya mechi ya Ruvu Shooting dhidi
ya Kagera Sugar, mwezi uliopita, kuna tiketi zilizoonyesha kuwa zinatakiwa
kuuzwa kwa Sh 3,000 lakini ziliuzwa kwa Sh 2,000, gazeti hili lilipouliza
wahusika hakuna aliyekuwa na jibu.
Kuna mashabiki wachache waliokuwa
wamekaa nyuma ya lango la upande wa magharibi waliokuwa wakivuta ‘sigara kubwa’
na hakukuwa na hatua zozote walizochukuliwa wala kuzuiliwa.
Lango kuu la kuingilia uwanjani hapo
ni la bati na halina ubora mzuri. Kwa hali halisi kuna sababu nyingi za TFF
kushirikiana na wamiliki wa viwanja kuendelea kuboresha viwanja ili viendane na
hadhi ya ligi husika.
Angalia vizuri picha na uone hali
ilivyo mbaya katika uwanja huo, hakika si hali nzuri na imepitiliza. TPL, hebu
fanyeni ziara au tumieni picha hizo kuona maana inawezekana mlipitiwa tu!







0 COMMENTS:
Post a Comment