Kwa mara ya kwanza baada ya kutua nchini na kujiunga na kikosi cha Simba, kiungo mpya wa timu hiyo, Kakule Mighuen Fabrice raia wa DR Congo, juzi Jumatatu alianza mazoezi kwenye timu hiyo na kuonyesha uwezo mkubwa huku mashabiki wao wakiwapiga vijembe watani wao Yanga kuwa watapata tabu sana msimu ujao.
Kiungo huyo, alianza mazoezi ya timu hiyo juzi Jumatatu jioni baada ya kutua nchini kwa ajili ya kusaini mkataba wa kuichezea Simba baada ya kaimu kocha mkuu wa timu hiyo Mrundi, Masoud Djuma kumpendekeza katika usajili wake.
Fabrice wakati wowote atasaini mkataba kama wakifikia muafaka mzuri na muwekezaji wa timu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’.
Katika mazoezi hayo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Boko Beach Veterani jijini Dar es Salaam, Fabrice anayecheza nafasi ya kiungo namba 6 na 8 alionyesha kiwango cha hali ya juu katika upigaji wa pasi, kukontroo na kukokota mpira na kutengeneza nafasi za mabao huku akipiga pasi za visigino hali iliyosababisha mashabiki waliojitokeza mazoezini hapo wamshangilie na kumpigia makofi kwa kumsifia.
Kiungo huyo ambaye ujio wake uliripotiwa kwa mara ya kwanza na Championi akitokea klabu ya Kiyovu Sports ya Rwanda alionyesha makali yake baada ya kocha Djuma kumtaka kuanza mazoezi kwa saa mbili sawa na dakika 120, huku akisubiria kusaini mkataba.
Akiwa uwanjani hapo Mcongo huyo ambaye ujio wake umefanywa na kocha wa timu hiyo, Masoud Djuma alionyesha uwezo kwenye kupiga pasi ambapo wakati mazoezi yanaanza hadi yanamalizika alipiga pasi 32 na tano pekee ndiyo alipoteza huku 27 zikiwafikia wenzake na yeye akifanikiwa kupokonya pasi mbili za wapinzani.
Mcongo huyo hakuishia hapo kwani alizidi kuonyesha yupo vizuri baada ya kutengeneza nafasi nne za mabao na akipiga mashuti matatu hali iliyoonyesha kuwakosha mashabiki wengi waliojitokeza katika mazoezi hayo. Kiungo huyo hakuishia hapo kwani alionyesha yumo kwa kuonyesha makeke ya kuwapiga tobo na kanzu wapinzani wake pamoja na kutumia msuli pale ambapo alienda kupambania mpira.
Kila zoezi ambalo lilikuwa linatolewa na kocha Djuma, kiungo huyo alifanya kwa kiwango cha juu ikiwemo kukimbia kwa spidi, mazoezi ya viungo pamoja na mechi ya muda mfupi ambayo ilivigawa vikosi viwili. Kikosi chake kiliundwa na Moses Kitandu, Abdul Suleiman, Mohamed Rashid, Mohammed Ibrahim na yeye Fabrice.
Mara baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, Djuma maarufu kama Irambona, alimuelezea kiungo huyo ambapo alisema: “Kiungo huyo kwa sasa yupo kwenye mazungumzo na uongozi wa Simba na kama akifanikiwa kukubaliana na viongozi wa Simba atasaini mkataba wa kuanza kuitumikia timu yetu.”
“Kitu ambacho kitakachomzuia Fabrice asisaini Simba labda afeli kwenye vipimo atakavyofanyiwa kabla ya kusaini, lakini kuhusu kiwango mimi kama kocha sina shida naye kwani ni mchezaji niliyewahi kukaa naye nikimfundisha kwa kipindi cha miaka mitatu,”alisema Djuma ambaye mashabiki wa Simba wametokea kumkubali zaidi.
CHANZO: CHAMPIONI
Jamani chama langu la msimbazi vipi tena? Nasikia huyu mkongomani bado ana mkataba unaoisha mwakani mwezi wa 7. Timu yake anayoichezea sasa hivi Kiyovu Sports ya Rwanda inataka kuipeleka Simba Fifa kuilalamikia kufanya mazungumzo na kumfanyisha mazoezi mchezaji wao ambaye bado ana mkataba....Jamani ehe pamoja na kwamba tuna shida ya wachezaji wa kigeni lakini tufanyeni mambo kwa weledi kidogo tusije kuingia kwenye matatizo, na hizi pesa za mwekezaji zitumiwe vizuri sio kwa pupa. Haya mambo kama ni kweli basi Simba tutaumia kweli na mkono wa Fifa
ReplyDeleteJamani chama langu la msimbazi vipi tena? Nasikia huyu mkongomani bado ana mkataba unaoisha mwakani mwezi wa 7. Timu yake anayoichezea sasa hivi Kiyovu Sports ya Rwanda inataka kuipeleka Simba Fifa kuilalamikia kufanya mazungumzo na kumfanyisha mazoezi mchezaji wao ambaye bado ana mkataba....Jamani ehe pamoja na kwamba tuna shida ya wachezaji wa kigeni lakini tufanyeni mambo kwa weledi kidogo tusije kuingia kwenye matatizo, na hizi pesa za mwekezaji zitumiwe vizuri sio kwa pupa. Haya mambo kama ni kweli basi Simba tutaumia kweli na mkono wa Fifa
ReplyDeleteGhafla nimemkumbuka Kanu Mbiavanga
ReplyDeleteChama langu nguvu mojaaa
ReplyDelete