Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
limetangaza rasmi utumiaji wa tiketi za elektroniki zitakazoanza kutumika
kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara utakaoanza Januari 25.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini
Dar es Salaam, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alitoa ufafanuzi juu ya
upatikanaji wa tiketi hizo ambapo aliwasisitiza wanunuzi kwamba watapata tiketi
hizo kupitia njia kuu tatu ambazo ni M-PESA
kwa kupiga *150*03*02#, njia ya CRDB Simbanking ambapo atapiga namba
*150*03# na kwa njia ya Fahari Huduma ambapo atapatiwa namba ya tiketi.
Aidha, alisema kuwa tayari tiketi hizo
zilikwishaanza kujaribiwa katika mechi ya kirafiki baina ya Azam FC dhidi ya
Ruvu Shooting katika Uwanja wa Chamazi kabla ya mechi nyingine itakayopigwa leo
kwenye uwanja huo kati ya JKT Ruvu na Ashanti United.
Aliongeza kuwa baada ya mteja kufanya
muamala huo, atakwenda katika vibanda maalum vya kutolea tiketi (uchapishaji)
akiwa na namba ya tiketi aliyonunua kwa kutumia njia mojawapo kati ya hizo
tatu. Lakini mteja atakatwa kiasi cha Sh 500 akitumia M-PESA na Sh. 300
akitumia njia ya CRDB.
“Baada ya kununua tiketi hiyo, mteja
atakwenda katika vibanda maalum vya uchapaji wa hizo tiketi akiwa na namba yake
ya tiketi,” alisema Wambura na kuongeza
kuwa tiketi hizo hazipatikani pale uwanjani. Kuna vituo maalum ambapo
zitakuwa zinapatikana na si uwanjani.”
0 COMMENTS:
Post a Comment