Kipa wa Simba, Ivo Mapunda,
amewataka wachezaji wenzake na timu nyingine kwa jumla kuwa makini na mabingwa
wa kihistoria wa Kenya FC Leopards katika michuano ya Mapinduzi
itakayofunguliwa leo Visiwani Zanzibar.
Simba itaanza mbio hizo kwa kuwavaa
Wakenya leo kabla ya kukutana na mabingwa wa Visiwani KMKM na Kampala City
Council KCC kwenye Kundi B.
Aidha, Mapunda anaifahamu vyema Leopards
kwani ni mahasimu wakubwa wa timu yake ya zamani ya Gor Mahia kabla ya kusaini
Simba dirisha dogo msimu huu.
Akizungumza na Championi Jumatano alisema
Leopards ya mwaka huu ni tishio kutokana na usajili waliofanya dirisha hili na
kusema si Simba inayotakiwa kuwa makini bali ni wito kwa timu zote.
“Kikweli kwa usajili waliofanya dirisha
hili, Leopards siyo ya kubeza, tunatakiwa kujiweka fiti hasa. Niliwaona wakati
wa mechi yangu ya mwisho nikiwa Gor Mahia (Ngao ya Hisani), hakika wameongeza
kitu fulani. Timu zinatakiwa kuwa makini nao na hata sisi ndiyo maana tunajifua
zaidi. Nawajua vyema,” alisema kipa huyo
wa zamani wa Yanga na African Lyon.
0 COMMENTS:
Post a Comment