January 1, 2014




Na Saleh Ally
UBISHI mkubwa ulikuwa ni kuhusiana na Arsenal kwamba kweli inaweza kuvuka Krismasi ikiwa bado kileleni mwa Ligi Kuu England maarufu kama Premiership? Imewezekana.
 
Baada ya hapo ikaonekana huenda mambo yakawa mambo, kwamba Arsenal inaweza isimalize mwaka 2013 bado ikiwa kileleni, kwa mara nyingine kikosi hicho cha Arsene Wenger kimefanikiwa kuvuka kikiwa kileleni.

Arsenal imeendelea kubaki kileleni ikiwa na pointi 42, inafuatiwa na Manchester City ambayo wamekuwa wakiona kama ‘watoa roho’ kutokana na kasi yao ya kufunga mabao, wana pointi 41, Chelsea ya Mourinho iko katika nafasi ya tatu na pointi 40.

Nyingine zilizo katika tano bora ni timu mbili za Jiji la Liverpool ambazo ni Everton yenye pointi 37 ikifuatiwa na Liverpool yenyewe yenye 36.
Hisia za wengi kwamba Arsenal itashindwa kuvumilia mikiki hadi Krismasi imetokana na rekodi karibu misimu minne kwa timu hiyo ya Wenger kushindwa kuwa katika nafasi hiyo.
Rekodi kadhaa za Premiership zinaonyesha timu ambayo huwa kileleni hadi Krismasi, yaani Desemba 25, imekuwa na nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa.
Bado inaonekana kwa Arsenal hilo linaweza kushindikana na kama litawezekana basi litakuwa ni kwa ugumu sana na hii ni kutokana na mwenendo wake.
Ukiangalia mechi sita kabla ya ile dhidi ya Newcastle iliyoshinda bao 1-0, utaona ilikuwa kileleni kwa tofauti zaidi ya pointi 8. Lakini kwa wiki nne, zimeporomoka haraka na anayefuatia ana tofauti ya pointi moja tu dhidi yao.
Kweli Arsenal imevuka Desemba 25 na imeingia mwaka mpya ikiwa kileleni, hofu ni namna ambavyo inaweza kuhimili vishindo vya timu ambazo zinaonekana kubadili gia na kupanda juu kwa kasi. 

Man City:
Inapanda kwa kasi zaidi, inaonekana kuwa na kikosi imara zaidi katika Premiership kwa kipindi kwa maana ya takwimu za mabao ya kufunga na kufungwa.

Katika mechi 19, Man City imefunga mabao 54 na kuweka rekodi ya timu yenye mabao mengi zaidi katika ligi zote kubwa barani Ulaya hadi mwaka 2013 unafungwa, imefungwa 21 tu.
Wastani wa kufunga mabao kwa mechi umekwenda hadi 3-0 kwa kuwa imeshinda mechi nyingi kwa idadi kubwa bila ya kujali inapambana na nani.

Chelsea:
Haishindi mabao mengi sana, lakini inaonekana Mourinho anakwenda na mfumo wa umuhimu wa pointi tatu kwanza. Utaona imefunga mabao 35, mawili chini ya Arsenal, lakini tayari imekwea nafasi ya tatu hata kabla ya mwaka kwisha.
Kutokana na mfumo wa hesabu za Mourinho na kwa kuwa ana kikosi kipana kwa maana ya kuwa salama hata kama kutakuwa na majeruhi, basi Arsenal hawako salama kileleni.

Liverpool:
Waliona wapinzani wa Arsenal, wamegombea kileleni lakini kabla ya mwaka mpya wametupwa nafasi ya tano baada ya kipigo cha Chelsea cha 2-1. Lakini bado si wa kuwadharau ingawa wanaweza kuwa funzo kwa Arsenal kwamba hata wao wanaweza kuangukia walipo Liverpool kama watazubaa kidogo tu.

Man United:
Wako nafasi ya sita, wanaonekana kama si hatari hivi. Lakini hesabu zinaonyesha bado ni tishio na wana nafasi ya kukwea kileleni baada ya mechi tano au sita tu.
Tofauti yao na Arsenal ni pointi nane tu, unaweza kusema ushindi wa mechi mbili na ushee. Lakini kubadilika kwa mwenendo wao na kushinda mechi nne mfululizo, maana yake wanakuja, wanapanda.
Ukiangalia katika timu sita za juu kwenye msimamo huo, timu zilizoshinda mechi nne mfululizo ni Man City na Man United tu, Arsenal imeshinda mechi mbili mfululizo sawa na Chelsea, Everton mechi moja na Liverpool imepoteza mbili baada ya kuwa imeshinda nne mfululizo.

Zifuatazo:
Premiership inarudi mzigoni leo, ndiyo mwaka mpya na Arsenal itauanza ikiwa nyumbani Emirates dhidi ya Cardiff City. Baada ya hapo itarejea dimbani Januari 13, ugenini dhidi ya Aston Villa, halafu Januari 18 nyumbani tena kuwakaribisha Fulham.

Arsenal itaumalizia Januari kwa kucheza tarehe 28 dhidi ya Southampton ikiwa ugenini. Ukiangalia kwa mechi hiyo, kama Arsenal itakomaa basi si zile zenye ‘hedeki’ na huenda ikaendelea kubaki kileleni tena kwa mwezi mzima kabla ya kuingia Februari.

Februari inaweza kuwa mtihani mkubwa kwa Arsenal kwa kuwa inakutana na timu ngumu ambazo ni Liverpool, Manchester United na pointi hizo sita inabidi kukomaa kweli ‘kibingwa’.
 


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic