Chama cha Makocha
Tanzania (Tafca), kimesema makocha wa kigeni wakiwemo wale wa Simba na Yanga,
hawatakaa kwenye mabenchi ya timu zao wakati wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba sasa inafundishwa
na Zdravko Logarusic raia wa Croatia na Yanga imempata Hans van Der Pluijm
kutoka nchini Uholanzi.
Tafca imelipitisha suala hilo
na kusisitiza kama klabu hizo hazitawasilisha nyaraka zao na kuwasajili makocha
hao, basi hawataruhusiwa kabisa kukaa kwenye benchi wakati timu zao zinashiriki
Ligi Kuu Bara.
Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), nalo liungana na Tafca na kusema walichosema Tafca ni kanuni na
kinapaswa kutekelezwa.
Katibu Mkuu wa Tafca, Michael Bundala, amesema wanachofanya ni kufuata
kanuni zilizowekwa na (TFF).
“Mzunguko wa pili unaanza
Januari 25, kama Simba, Yanga na timu nyingine watakuwa hawajawasajili makocha
wao, wasahau kuwatumia.
“Hatutakuwa na mzaha,
hatuwezi kukubali washiriki katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara,” alisema
Bundala.
Maana yake kama Simba
watafanya uzembe, Logarusic ataishuhudia Simba akiwa jukwaani kama ilivyo kwa
van der Pluijm na Yanga.
Bundala alisema kanuni ya
61 ya TFF inayozungumzia makocha wa ligi kuu, inasema ni lazima makocha wa
kigeni wanaokuja kufanya kazi hapa nchini watambuliwe na Tafca kabla ya kuanza
kufanya kazi zao.
“Safari hii hatutaki
mchezo, tayari tumeshaiandikia barua TFF tukiitaka izingatie kanuni na taratibu
zake ilizojiwekea kwa faida ya soka la Tanzania,” alisema Bundala na kuongeza:
“Mpaka sasa hakuna kocha
yeyote wa kigeni anayetambuliwa na chama, hawataruhusiwa kufundisha timu hizo
ligi itakapoanza.”
Kuhusiana na hilo, Ofisa
Habari wa TFF, Boniface Wambura, alipoulizwa kama wameipata barua hiyo ya Tafca
alisema:
“Bado hatunaiona hiyo
barua, lakini suala hili ni la kikanuni, hivyo lazima litazingatiwa.”
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment