Kocha Msaidizi wa Mbeya City, Maka
Mwalwisye, ametaja kilichoiua timu hiyo katika michuano ya Kombe la Mapinduzi
kuwa ni waamuzi.
Kocha huyo amesema uamuzi kwenye
michuano hiyo ulikuwa mbovu na wengi wao walikuwa hawafuati sheria 17 za soka.
Mbeya City juzi ilishindwa kutamba mbele
ya timu ya URA ya nchini Uganda baada ya kuchapwa bao 1-0 na kushindwa kuingia
katika robo fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Akizungumza na Championi Jumatano, kocha
huyo alisema katika michuano hiyo kwa jumla waamuzi hawakuwa makini katika
kutoa maamuzi, tena kwa kushindwa kuzingatia sheria.
Maka alisema, hata hivyo, wachezaji wa
timu yake wamejifunza mengi kutokana na michuano hiyo na imeweza kuwasaidia
kujiimarisha zaidi kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Uamuzi ulikuwa mbovu kutokana na
kutozingatia sheria za mchezo, kitu kilichochangia hata timu kushindwa kufanya
vyema kutokana na refa kutokuwa makini katika kuangalia nini anafanya pale
uwanjani.
“Lakini kwa upande mwingine tumejifunza
mengi na tumegundua wapi tunahitaji kurekebisha kabla ya kuanza mzunguko wa
pili wa ligi na tuseme tumeweza kupata hata mechi kubwa kama kucheza na URA ya
Uganda ambacho ni kipimo tosha kwetu.
“Na kwa jumla mashindano haya yametupa
mwanga katika kuelekea mzunguko wa pili, japo tulikuwa hatujajiandaa kwa muda
mrefu kwa sababu wachezaji ndiyo kwanza walikuwa wakitoka katika mapumziko,” alisema
Maka.
0 COMMENTS:
Post a Comment