WAKATI
fulani nilikuwa nchini Ujerumani, niliishi kwa takribani wiki tatu kwenye mji
mdogo tu wa Freiburg ambao ndiyo mji mkubwa zaidi kusini mwa nchi hiyo.
Mji huo una
raha moja, pamoja na kwamba si mkubwa kama ilivyo Berlin, Munich, Frankfurt na
mingine ambayo nimewahi kutembelea, una
bahati ya kuwa karibu na nchi mbili, Ufaransa na Uswisi. Hivyo inakuwa ni rahisi
sana kuzifikia nchi hizo mbili.
Mmoja wa
rafiki zangu aliyekuwa anaishi Freiburg, alikuwa na mapenzi makubwa na timu yao
ya Freiburg FC ambayo tokea imepanda Bundesliga, hata mara moja haikuwahi kuwa
na ndoto hata ya kutwaa ubingwa wa Bundesliga na kucheza Ligi ya Mabingwa
Ulaya.
Ndoto ya
timu hiyo na mashabiki wake ni kuhakikisha inabaki kwenye Bundesliga, hivyo
mashabiki na wadau kwa ujumla wamekuwa wakifanya kila linalowezekana ili ndoto
yao itimie.
Ukimuuliza
kwa nini msianze kuwaza kuchukua ubingwa wa Bundesliga, jibu lake: “Mashabiki
wa Freiburg FC ni waelewa, wanajua kulazimisha kubeba ubingwa ni sawa na
binadamu kung’ang’ania kupaa hewani, haiwezekani kwa kuwa hatuna mabawa. Siku
ikifika, basi timu ifanye hivyo na sisi tutaiunga mkono.”
Wanaiunga
mkono vipi kwa sasa: “Kwa kuwa tunaona ina uwezo wa kubaki Bundesliga, basi
juhudi zetu ni kuiunga mkono kwa kutoa fedha pamoja na kuishangilia uwanjani.”
Unajua
wanavyotoa fedha? Ngoja nikuelezee, kwanza ni kuhakikisha wananunua vitu, mfano
jezi, vibeba ufunguo na bidhaa nyingine za timu hiyo. Halafu wananunua tiketi
za mechi zao kwa wingi ili kuhakikisha haipati hasara.
Lakini
ajabu wao pia wanawaunga mkono hata wadhamini wanaoipa sapoti Freiburg FC ili
wasijute na kujua walikosea kuidhamini timu hiyo kutoka Kusini mwa Ujerumani.
Kazi yangu
si kuhamasisha watu wanunue bidhaa za wadhamini wa timu za ligi kuu, hilo ni
chaguo lenu, pia najua hamwezi kununua jezi na vifaa orijino vya Yanga na Simba
kwa kuwa hata klabu zenyewe hazina mpango wa kuviuza na wajanja wanaendelea
kujifaidisha.
Lakini
ninaamini mnaweza kuziunga mkono klabu zenu, kwanza kwa kulipa ada za uanachama
kwa ufasaha, lakini pia kuna suala moja, nendeni viwanjani zinapokuwa
zinacheza, lipeni viingilio ili timu ziweze kupata faida na kujiendeleza.
Viingilio
vyenu kama kutakuwa na udhibiti, vitaweza kusaidia klabu zenu kuwa na uwezo wa
kifedha, zinawalipa makocha, wachezaji, wafanyakazi wake, pia zitaweza
kujiendesha. Kwani hata klabu za Ligi kuu England, mapato ya milangoni ni kati
ya vyanzo vikuu vya mapato.
Mnataka mkae
nyumbani, timu zenu zinacheza viwanja vikiwa tupu, halafu mnadai mnazipenda au
kuziunga mkono? Huo ni uongo na kama
mapenzi huenda yakawa ni ya rangi na si yale ya dhati.
Angalia
namna mechi za Ligi Kuu Bara zilivyo na watu wachache na kadiri siku
zinavyosonga mbele, watu wamekuwa wakizidi kupungua viwanjani, hali
inayoashiria watu wengi kutojua maana ya kuziunga mkono timu zao.
Si Yanga na
Simba tu, hata wale wa Ashanti na timu nyingine zinazotegemea mapato ili
kuishi, lazima wajue msaada wao ni muhimu na kukaa kwenye vijiwe na
kuzizungumzia huku wengi wakilalama kuhusu kuwa na maendeleo duni bila ya
kuzichangia lolote, si sahihi.
Wanaozichangia
timu zao angalau wanaweza kuwa na uwezo wa kulaumu, na utaona mashabiki wengi
wa timu za mchangani wamekuwa na mapenzi makubwa na timu zao kuliko hata wale
wa Simba na Yanga.
Wanakaa
barabarani kuchangisha, fedha zikipungua wanafanya kila liwezekanalo
kuchangisha hata kuwalipa wachezaji mahiri wanaokodishwa kuzisaidia timu zao.
Lakini mashabiki wa timu kongwe wanasubiri kulaumu tu. Hiyo si sahihi, mjipime,
halafu badilikeni.








0 COMMENTS:
Post a Comment