Na Saleh Ally
SIKU chache zilizopita nilikwenda kwenye mazoezi ya
Simba kwenye Uwanja wa Kinesi eneo la Shekilango jijini Dar es Salaam. Lengo
lilikuwa ni kuangalia kazi za kocha Zdravko Logarusic kwa ajili ya kujifunza.
Mimi si mwalimu wa soka, lakini napenda kujifunza
kupitia kila anayejua. Mara nyingi nimekuwa nikifanya hivyo asubuhi, lakini
nikaona si vibaya nikienda hata katika mazoezi ya jioni, maana nilielezwa Simba
hawafanyi mazoezi asubuhi.
Dakika chache baada ya kuingia kwenye mazoezi ya
Simba, kuna baadhi ya mashabiki walianza kunizomea na kutoa maneno makali,
kiasi fulani ilinishangaza lakini sikuwa na hofu hata kidogo kwa kuwa nimekuwa
sugu na ninapenda kuishi nikijifunza.
Ukikutana na watu wa namna hiyo ni nafasi ya
kukuonyesha namna gani Mwenyezi Mungu ameumba watu wa aina tofauti. Waelewa na
wasio waelewa, lakini wasiojitambua kwa hali waliyonayo.
Waliokuwa wakitukana matusi ya nguoni walisema hivi:
“Nenda kwenu Zanzibar huko, si umewapa Yanga Okwi, sasa wape na Kapombe kabisa
ili ufurahi. Kazi yako ya uwakala wa soka siyo hapa, kama unataka wafuate Yanga
Bagamoyo ukafanye huo uwakala.”
Maneno yaliyokuwa yakisemwa huku yakiambatana na
matusi makali kabisa, yalinishangaza kidogo. Saleh Ally anaweza kuwapa Yanga
Okwi? Kivipi? Anaweza kuwapa Kapombe kwa njia ipi? Lakini nikaona haikuwa
busara kwangu kuendelea kufikiria wanachosema, badala yake nifuate
kilichonipeleka mazoezini.
Wakati nikiwa mwandishi chipukizi, nakumbuka baadhi ya
viongozi walikuwa wakiwapanga mashabiki kuzomea waandishi waliowakosoa kila
wanapokwenda mazoezini. Hivyo huenda mimi nina ‘zomea proof’ mwilini mwangu.
Hilo haliwezi kunipa shida.
Nakumbuka mwaka 2008 wakati nikiwa mwandishi wa gazeti
la Mwanaspoti, nilikwenda kwenye mazoezi ya Yanga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM) nikiwa na ‘kijana wangu’, Michael Momburi. Baada ya kufika pale, Kocha
Jack Chamangwana aliniita na kutaka kunisaidia, nikaanza kumuuliza maswali,
muda wote huo, mashabiki wa Yanga waliendelea kuzomea.
Wakati natoka wapo walioanza kutoa vitisho, hali hiyo
ilimtisha Momburi, akazidi kuongeza mwendo. Mimi nikaona haikuwa sahihi,
nikasogea hadi kwenye lile kundi na kutaka kujua sababu. Walinieleza hoja zao,
nami nikawaambia niko tayari kuzijibu.
Hatua kwa hatua, wakaenda wanapungua, mwisho akabaki
mmoja na baadaye wote wakakubali haikuwa sawa kuzomea na wakati naondoka
nikapigiwa makofi.
Sijasahau hadi leo si kwa kuwa nilipigiwa makofi,
badala yake namna watu wale wazima walivyoshindwa kujenga hoja wakaamini
kuzomea na matusi ndiyo picha ya utu wao, lakini nikaamini wanaweza kubadilika
kwa kuamini hoja ni nembo ya binadamu anayejitambua.
Katika mazoezi hayo ya siku chache zilizopita,
niligeuka kuangalia waliokuwa wakizomea, niligundua hawakuzidi watu watatu,
haraka nikaangalia sura zao, nikawa nimepata somo. Naweza kusema niliona ni
watu wapenda sifa, wasio na upeo mzuri wa ufafanuzi wa mambo ambao wanaamini
kelele nyingi ni sehemu ya kutambulika au kujitambulisha.
Nikaendelea kukaa kimya, lakini baada ya muda
kikaibuka kichekesho. Mtu mmoja kati yao aliibuka na kuwaambia mnayemzomea ni
Saleh Ally, si Ally Saleh na huyo si wakala kama mnavyofikiri. Baada ya hapo
baadhi yao walianza kupunguza maneno.
Hapo ndipo niligundua kwamba waliamini mimi ni Ally
Saleh ‘Alberto’ wa Zanzibar, tena kumbe chuki kwake kwa kuwa siku chache
zilizopita alihojiwa na Maulid Kitenge wa Radio One na kueleza namna Yanga
ilivyokuwa na uhalali wa kumtumia Okwi.
Lakini bado nikajiuliza, hata ingekuwa hivyo yaani
ambaye angekuwa ameingia uwanjani pale kweli angekuwa ni Ally Saleh kweli
alistahili maneno ya matusi? Huyo shabiki au mashabiki wanaotukana hawajui
aliyesababisha yote hayo ni yupi?
Ally Saleh ana haki ya kuzungumzia anachokifahamu,
kama mashabiki wangekuwa na busara siku wakimuona, wangeweza kumuita na
kuzungumza naye kwa hoja kwa lengo la kujifunza. Kuropoka, kutukana, hakuwezi
kuwa ndiyo njia sahihi ya kujua au kufanikisha jambo.
Wewe usiyejua, unatakiwa kujifunza. Kama unamtukana
anayeweza kukusaidia kujifunza, basi maneno machafu ndiyo yatabaki kuwa
mwonekano wa picha ya jinsi ulivyo.
Na kama unaishi kwa kupata sifa kupitia matusi, basi
wewe ni mtu wa ajabu na vizuri ukajitambua. Nani amewahi kujenga au kutengeneza
kitu bora kwa kutumia lugha chafu za matusi?
Kama nilivyoeleza awali, hata baada ya kugundua
waliokuwa wakinitusi walidhani mimi ni Ally Saleh, sikuhitaji kuombwa radhi.
Maisha yangu yote ya utoto nimeishi nikicheza soka katika timu za mchangani na
matusi si tatizo kwangu.
Kiasi fulani niliona walikaa kimya baada ya kugundua
waliyekuwa wakimshambulia kwa maneno machafu hakuwa waliyekuwa wamemkusudia.
Lakini bado mimi nikawa nimejifuza tena kama
nilivyoeleza kuwa napenda kujifunza katika kila jambo.
Kwamba kama tumekuwa tukilalamikia utendaji wa
viongozi wa soka kuwa wazembe au wabinafsi, basi kuna kila sababu ya kuwafunza hata
mashabiki na wanachama wa klabu zetu kwamba bado wanahitaji kujifunza.
Huenda kujitambua ni jambo zuri, kama unafikia hadi
kumshambulia mtu ambaye si sahihi, maana yake wewe ni mtu wa kukurupuka na haufanyi
uchunguzi, mambo yako si ya uhakika na unakwenda kwa kupapasa. Sasa kama uko
hivyo, kweli utakuwa msaada kwa klabu yako?
Kama wewe unakwenda kwa kubahatisha, unaweza kumsaidia
mwingine au kuwa na mawazo ya kuisaidia klabu kujenga kitu cha msingi? Iko haja
ya wanachama au mashabiki kujifunza kuwa wanaoweza kujenga hoja za msingi
badala ya kukurupuka tu.
Kama tumekuwa tukilia na viongozi wanaoziangusha
klabu, basi hata wanachama matatizo wasiojitambua wanaweza kuwa tatizo pia na ukiwajumlisha
wao na viongozi tatizo, maana yake ni majanga kwenye klabu na hasa kongwe za
Yanga na Simba.
Kwa kuwa ushabiki haunipi shida, bila ya woga ilimradi
ninaamini ninachokifanya ni kwa lengo la kujenga, nitaendelea kusifia na
kukosoa bila ya woga hata kidogo.
Waandishi wengine walio tayari kutaka kusaidia michezo
nchini, wanapaswa kutohofia maneno kama yale ya mashabiki, badala yake
wapiganie michezo ya Tanzania.
Tuko nyuma sana, tunaachwa na kila mtu na tukiwa waoga
na kuwapa nafasi wanaokurupuka kama wale mashabiki, tutakwama hapa milele, kitu
ambacho si sahihi hata kidogo.
Pamoja na hivyo, huu ni wakati mzuri kwa mashabiki wa
soka hasa wa Yanga na Simba kutafakari, kipi mnaona sahihi. Kuendelea kuishi
kwa kubahatisha na kupata sifa za umaarufu kuwa mnaweza kukurupuka na kutukana
au muwe wajenga hoja, mnaochambua mambo ili inapofikia mnataka kumkosoa mtu,
basi muwe na uhakika.
Salamu kwenu.
0 COMMENTS:
Post a Comment