Na Saleh Ally
MIAKA minne iliyopita,
mshambuliaji Mbwana Ally Samatta hakuwa na umaarufu wowote katika soka hapa
nyumbani zaidi ya kusikika kwa mbali wakati akiitumikia timu yake ya African
Lyon.
Lyon iliyokuwa ikimilikiwa
na mfanyabiashara maarufu Mohammed Dewji ‘Mo’ ilikuwa ikipambana kupanda Ligi
Kuu Bara, kipindi hicho kinda Samatta hakuwa maarufu lakini kwa aina ya
uchezaji wake na msaada mkubwa kwa timu yake, taratibu jina likaanza kupanda.
Msimu mmoja tu baada ya kushiriki
Ligi Kuu Bara, Dewji aliamua kuiuza timu hiyo na baadaye kumuacha Samatta aende
Simba ambayo aliitumikia kwa msimu mmoja tu kabla ya kuuzwa TP Mazembe ya DR
Congo.
Muda huo mchache sasa
Samatta ni mmoja wa wachezaji ghali barani Afrika na ndiye anayelipwa kuliko
wote wanaocheza soka kutoka Tanzania, bila ya kujali wako barani Afrika, Asia
au Ulaya.
Mshahara wa Samatta na TP
Mazembe kwa mwezi ni dola 10,000 (zaidi ya Sh milioni 16), maana yake mshahara
wake unaweza kuwalipa wachezaji wa timu moja ya Ligi Kuu Bara kwa mwezi.
Mfano ni timu za jeshi
kama JKT Ruvu, Ruvu Shooting, JKT Oljoro na nyinginezo, lakini timu kama
Ashanti ni kati ya zile ambazo mshahara wa mwezi wa Samatta unaweza kuwalipa
wachezaji wao kwa asilimia 90 au 100 kabisa.
Lakini mshahara pekee
hautoshi kuonyesha mabadiliko ya haraka sana ya Samatta, vitu vingine vikubwa
viwili ni thamani anayopewa kwa kipindi hiki kuwa imefikia dola pauni 450,000
(zaidi ya Sh bilioni 1.2).
Hakuna mchezaji wa
Tanzania ambaye aliwekwa kwenye soko kupitia mitandao maarufu ya mauzo ya
wanasoka na akafikia thamani ya Samatta.
Hiyo haitoshi, kuonyesha
kuwa thamani hiyo si uongo, Klabu ya Al Ain inayoshiriki Ligi Kuu ya Falme za
Kiarabu ((UAE), tayari iko tayari kutoa dau la dola milioni 1 (zaidi ya Sh bilioni
1.6) ili kumnasa Samatta akakipige kwenye timu yao.
Samatta ni kijana wa
Mbagala ambaye hakuwa na umaarufu wa juu kama Mrisho Ngassa, Athumani Iddi
Chuji, Haruna Moshi ‘Boban’ lakini alipofikia ni hatua nyingine kabisa ambayo
ina mambo mengi ya kujifunza.
Hana digrii wala
‘mastaz’, lakini mshahara wake ni maradufu wa ule wa bosi wa benki, mhasibu
mkuu wa wizara na hata mawaziri.
Samatta ni tishio kwenye
Ligi ya Mabingwa Afrika, timu yoyote, zikiwemo Al Ahly, Zamalek, Orlando
Pirates, Esparance na nyingine kubwa zikisikia zinakutana na TP Mazembe, basi
mahesabu yanaanzia namna ya kumzuia.
Kujivunia Samatta kwa
kila Mtanzania bila ya kujali ushabiki ni jambo zuri, lakini litakuwa ni jambo
jema zaidi kama kumbukumbu ya alikopita na alipofikia ndiyo ikawa njia sahihi
zaidi ya kujivunia na kujifunza pia.
Kufikia alipo Samatta
kunaonyesha kuwa Tanzania ina wachezaji wengi sana wenye vipaji vinavyoweza kudhihirisha
ubora wao kwa kiasi kikubwa.
Lakini kumekuwa na dharau
kwa kuwa bado imani iko juu sana kwamba hakuna anayeweza kufanikiwa kama mastaa
walio Simba, Yanga au Azam kwa kipindi hiki, lakini Samatta amewapita kama
upepo wa kimbunga, na sasa wanamsoma kwa mbali mno.
Pia, kumekuwa na viongozi
wenye roho ya husda wasiotaka kuwaona vijana wengine wakifanikiwa kwa maslahi
yao binafsi, au wakiamini mchezaji akiondoka Simba au Yanga itadhoofika, hivyo
wanamlaghai, anabaki na miaka miwili anaonekana hana maana na inabidi wanaachane naye.
Samatta amefanikiwa
kupiga hatua kubwa sana katika miaka minne tu, kati ya hiyo miwili na ushee
akiwa na TP Mazembe. Sasa ndiye staa wa TP Mazembe, Lubumbashi na DR Congo
yote. Wako wengine wanaoweza kupita wakafika mbali, basi wajitume lakini
viongozi wapeni njia kama Simba walivyokubali kwa Samatta kuliko kuendelea kuwang’ang’ania
vijana na mwisho, mnawatupa kama matambala ya deki.
Samatta Data:
Ndoa na TP Mazembe:
Miaka 2, Miezi 7, Siku 6
Ligi ya Mabingwa
Mechi 17
Mabao 9
Kufuzu Kombe la Dunia:
Mechi 7
Mabao 2
Kufuzu Can:
Mechi 5
Mabao 2
Fin.
0 COMMENTS:
Post a Comment