Na Saleh Ally
HUU ni wakati wa mateso ya moyo kwa mashabiki wa Manchester
United. Inawezekana wako watakaokataa kwa hisia lakini hali halisi inaonyesha
hivyo.
Wataendelea kuteseka hadi mambo kadhaa yatakapobadilika ili kuweka
mambo sawa.
Mabadiliko makubwa yanatakiwa kuanzia kwa Kocha Mkuu, David Moyes,
maarufu kama Daudi kwa mashabiki wa soka hapa nchini. Lazima aonyeshe kujiamini na kuna mambo muhimu
yanatakiwa kuanzia kwake kabla ya wengine.
Katika mechi ya Ligi Kuu England kati ya Arsenal dhidi ya Man
United, wachezaji wa Man United walionyesha wazi kwamba hawakuwa wakicheza kwa
juhudi kwa asilimia mia. Hata kama walifanya hivyo ilikuwa kwa kipindi fulani.
Mambo mengi yanapaswa kubadilishwa katika kikosi hicho, huenda kwa
sasa ikaonekana kuna wachezaji ambao hawana uwezo mzuri, lakini kama hali ya
kisaikolojia haitakuwa vizuri, bado hata wapya watakaosajiliwa watashindwa
kufanya vema.
Moyes anaweza kuanza na suala la kiungo nyota mshambuliaji, Adnan
Januzaj, ambaye ana kila sababu ya kumuamini na kumtumia kwa ajili ya kumjenga
na ana uwezo wa kukisaidia kikosi chake kuleta mabadiliko.
Awali, Moyes alionyesha hilo kwa Januzaj lakini kadiri siku
zinavyosonga mbele, amekuwa akimuingiza akitokea benchi, huku akiamua kumtumia
mkongwe kama Ashley Young ambaye inaonekana uwezo wake umeporomoka, na jibu
lingekuwa ni kinda huyo.
Kocha aliyepita wa Manchester United, Alex Chapman Ferguson,
alifanya mambo kadhaa ambayo Moyes anaweza kujifunza na yatamsaidia kubadilisha
mambo kadhaa, jambo zuri kwake kama mfano ni lile la Cristiano Ronaldo.
Ronaldo hakuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza cha Sporting Lisbon,
tayari makocha kadhaa kama Arsene Wenger wa Arsenal na Gerard Houllier wa
Liverpool wakati huo walikuwa wameishaanza kumuona lakini Ferguson akaonyesha
kuwa ni kocha mwepesi kuchukua uamuzi.
Kwani Manchester United ilipocheza na Sporting Lisbon jijini
Lisbon na kufungwa mabao 3-1 katika mechi ya kirafiki, Ferguson alimchangamkia
mapema kinda huyo.
Ingawa wengi wanaamini kelele za wachezaji wake kutaka amsajili
wakiwa kwenye ndege wanarejea England zilichochea hilo, lakini ukweli ni hivi: Hata
kabla ya mechi hiyo, Ferguson alizungumza na uongozi pamoja na Ronaldo na
walikuwa wamemalizana.
Siku chache baadaye Ronaldo alifunga safari kwenda
Manchester akiongozana na wakala wake na huko alisajiliwa kwa dau la pauni
milioni 15 (Sh bilioni 35) na utaona haikuchukua hata siku tano kabla hajaanza
kumchezesha, na kingine kikubwa alichokifanya ni kuonyesha anajiamini.
Baada ya kumaliza kila kitu, Ferguson alimuuliza Ronaldo
alipendelea jezi ya aina gani. Yeye alisema anataka apewe jezi namba 28, ambayo
alikuwa akiitumikia wakati akiwa Sporting Lisbon. Alihofia kuivaa jezi namba 7,
ambayo mara ya mwisho ilikuwa ikivaliwa na David Beckham ambaye aliondoka na
kujiunga na Real Madrid.
Beckham alikuwa nyota kuliko mchezaji mwingine England
wakati huo, lakini kabla, jezi hiyo ilivaliwa na magwiji kama Eric Cantona na
Bobby Charlton, hivyo Ronaldo alikuwa na haki ya kuihofia. Lakini angalia
Ferguson alivyomjengea hali ya kujiamini, alisisitiza: “Utavaa jezi namba saba,
achana na hiyo 28.”
Kumpa Ronaldo jezi namba saba, hakuna ubishi ulikuwa mzigo
mkubwa. Lakini fomula inasema hivi: Binadamu akipewa kitu kigumu zaidi ndiyo wakati
wa uwezo wake kuonekana.
Maana yake Ronaldo aliona ana deni kubwa mbele yake,
akaweka juhudi zaidi kusudi asifeli au kuaminika kwa kuwa kila aliyekuwa na
jezi hiyo alifanya vizuri kwa kipindi kirefu na kuwa ‘anayeibeba’ Manchester
United.
Moyes anasubiri nini kwa Adnan Januzaj, kinda anayeonekana
kuwa na kila kitu kasoro vitu viwili tu! Kupewa nafasi ya kucheza na kuaminiwa,
basi. Uwezo na kipawa cha juu anacho, sasa vipi Moyes anashindwa kujiamini na
kumpa nafasi badala ya kuwa anamuingiza kipindi cha pili?
Rekodi zinaonyesha Januzaj amecheza mechi 19, kati ya hizo
10 pekee ameanza na tisa ameingia. Amefunga mabao matatu, ametoa pasi mbili za
mabao na amepiga mashuti 36. Dalili kwamba ana uwezo, tatizo ni kuaminiwa, kitu
anachotakiwa kukifanya Moyes.
Moyes amekuwa akimuamini Young ambaye hata kama akifanya
vizuri kwa msimu huu, hana uhakika wa ubora wa juu katika misimu mingine
miwili. Vema nafasi hiyo akampa Januzaj ambaye kama atakuwa bora msimu huu,
basi ni faida kwake kwa misimu mingine hata mitano kama wataweza kumbakiza.
Januzaj ana kasi, uwezo wa kupiga mashuti, krosi na
msumbufu kwa mabeki. Huu ndiyo wakati mwafaka na ‘Daudi’ anapaswa kupunguza
uoga, kujiamini na kufanya kile kilicho sahihi bila ya kuhofia lawama.
Wakati Ferguson ameingia Manchester United mwaka 1986, akitokea
Aberdeen, miaka mitatu ilikuwa ya mateso kwake na mashabiki walikuwa wakiingia
uwanjani na mabango wakitaka aondoke, lakini kipindi hicho ndicho alikuwa
akitangaza kuwatema baadhi ya mastaa vipenzi vya mashabiki na akasisitiza
anajenga kikosi. Moyes anaweza pia kujifunza.
TAKWIMU:
MSIMU WA 2013-14
MECHI
MABAO PASI ZAO MASHUTI
19 3 2 36








0 COMMENTS:
Post a Comment