Stand United ya Shinyanga imekata
rufani Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikipinga Kanembwa JKT ya
Kigoma kuchezesha wachezaji waliosajiliwa katika dirisha dogo kwenye mechi ya
kiporo iliyozikutanisha timu hizo.
Mechi hiyo namba 22 ya Ligi Daraja la
Kwanza (FDL) ilichezwa juzi (Februari 16 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Ali Hassan
Mwinyi mjini Tabora ambapo Kanembwa JKT iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Katika rufani yake, Stand United
inadai kwenye mechi hiyo Kanembwa JKT ilichezesha wachezaji wanane
waliosajiliwa katika dirisha kidogo kinyume na maelekezo kutoka TFF kwa timu
hizo kuwa wachezaji waliosajiliwa katika dirisha dogo hawawezi kucheza mechi
hiyo.
Wachezaji wanaodaiwa kusajiliwa
dirisha dogo na kucheza mechi hiyo ni Hamidu Juma, Ibrahim Shaban Issa, Joseph
Mlary, Lucas Charles Karanga, Raji Ismail, Salvatory Kulia Raphael, Seif
Ibrahim Zaid na Yonathan David Sabugowiga.
Dirisha dogo lilifunguliwa Novemba 15
na kufungwa Desemba 15 mwaka jana, hivyo Stand United katika rufani yake inaombwa
ipewe pointi tatu na mabao matatu kwa Kanembwa JKT kuchezesha wachezaji
wasiostahili.
Awali mechi hiyo ilichezwa Novemba 2
mwaka jana Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, na kuvunjwa na mwamuzi dakika
ya 87 baada ya Kanembwa JKT kugomea pigo la penalti dhidi yao.
0 COMMENTS:
Post a Comment