February 21, 2014


Mechi ya pili ya raundi ya kwanza kuwania Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Tanzania (Twiga Stars) na Zambia (Shepolopolo) sasa itachezwa Februari 28 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.


Twiga Stars tayari ipo kambini kujiandaa kwa mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili jioni. Twiga Stars chini ya Kocha Rogasian Kaijage inafanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa Karume ambao ni wa nyasi za bandia kama ulivyo ule wa Azam Complex.

Shepolopolo iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Februari 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nkoloma jijini Lusaka.

Iwapo Twiga Stars itafanikiwa kuiondoa Shepolopolo itacheza na mshindi wa mechi kati ya Botswana na Zimbabwe. Zimbabwe ilishinda mechi ya kwanza ugenini.

Wachezaji wa Twiga Stars waliopo kambini ni Amina Ali, Anastazia Katunzi, Asha Rashid, Donisia Minja, Esther Chabruma, Etoe Mlenzi, Everine Sekikubo, Fatuma Issa, Fatuma Makusanya, Fatuma Mustafa, Fatuma Mwisendi, Fatuma Omari, Flora Kayanda, Happiness Mwaipaja, Maimuna Mkane, Mwajuma Abdallah, Mwapewa Mtumwa, Pulkeria Charaji, Sherida Boniface, Sophia Mwasikili, Therese Yona, Vumilia Maarifa na Zena Said.

MECHI TANO VPL KUCHEZWA JUMAMOSI
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi ya 19 kesho (Februari 22 mwaka huu) kwa mechi tano zitakazochezwa katika miji ya Dar es Salaam, Bukoba, Morogoro, Tanga na Arusha.

Yanga itakuwa mgeni wa Ruvu Shooting ya mkoani Pwani katika mechi itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Nayo Kagera Sugar inaikaribisha Rhino Rangers ya Tabora katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Uwanja wa Manungu uliopo Turiani mkoani Morogoro ndiyo utakaotumika kwa mechi kati ya Mtibwa Sugar na Ashanti United, wakati Coastal Union itaumana na Mbeya City katika mechi itakayooneshwa moja kwa moja na Azam Tv kutoka Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Maafande wa Oljoro JKT watakuwa nyumbani kupambana na Mgambo Shooting katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.

Jumapili (Februari 23 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa ni Simba dhidi ya JKT Ruvu, mechi ambayo pia itaoneshwa moja kwa moja na Azam Tv. Mechi kati ya Azam na Tanzania Prisons iliyokuwa ichezwe kesho (Februari 22 mwaka huu) Uwanja wa Chamazi sasa itachezwa Jumapili (Februari 23 mwaka huu) ambapo na itakuwa ‘live’.


Ligi hiyo itaendelea Jumatano (Februari 26 mwaka huu) kwa mechi moja kati ya Ashanti United na Azam itakayochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex (Chamazi).

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic