Na Saleh Ally
HII si mara ya kwanza kusikia mashabiki wa soka wamefanya
vurugu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kusababisha uharibifu
mkubwa kwenye vifaa vya uwanja huo.
Haraka labda nifanye hivi, napenda kuwakumbusha mashabiki na
watu wengine kuwa Uwanja wa Taifa ndiyo bora na wa kisasa zaidi kuliko vingine
vyote katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Nitakutakia nchi ili ukumbuke vizuri,
Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, DR Congo, Ethiopia na Sudan.
Inawezekana kwa kuwa mimi na wewe ni Watanzania, basi
tunakuwa wagumu kuamini kama kitu kikiwa Tanzania kinaweza kuwa bora kuliko
vilivyo sehemu nyingine, lakini kwa uwanja tulio nao, hiyo ndiyo habari
ninayokupa na kama ulikuwa unalijua hilo, si vibaya, nimekukumbusha.
Hao Al Ahly wanaotokea Misri, nchi liyoendelea sana kimatafa
katika michezo, hawa uwanja wao pamoja na kwamba ni mkubwa sana, lakini si bora
kama ulivyo huo wa Taifa ambao umefunikwa juu na ni wa kisasa kuliko wa kwao
ambao umekuwa ukiongezewa viraka mara kadhaa.
Kuna viwanja katika nchi mbalimbali barani Ulaya, pamoja na
kuwa maarufu havina ubora wa Uwanja wa Taifa, hakika Watanzania wana kila
sababu ya kujivunia na kuulinda uwanja huo. Lakini ajabu kabisa, kumekuwa na
makundi ya mashabiki wanaofanya juhudi za kuuharibu.
Takribani mechi nne, nimeshuhudia eti, mashabiki wenye hasira
kali wameamua kung’oa viti na kuwarushia wengine. Kitu ambacho kama umetuliza
akili zako, utaona kama ni ndoto au wanaofanya si watu wenye akili timamu
badala yake ni wenye matatizo kisaikolojia.
Suala hili si sahihi, mtu ambaye hatakiwi kung’oa viti hivyo
anapaswa kuonyesha upendo na uzalendo kwa mali za taifa lake, hadi asombe sifa
nilizozitoa kuhusiana na uwanja huo, badala yake anapaswa kujitambua.
Uwanja huo ni mali ya Watanzania, mimi, wewe na yule na
tunapaswa kujivunia, kuwa tuna kitu bora na tunapaswa kukitunza. Lakini ajabu
kila zinapotokea tafrani uwanjani, mashabiki hung’oa viti na kuanza kurushia,
vinahusika vipi.
Inakuwaje mtu mwenye hasira lazima ang’oe viti? Viti vinahusika
nini kati ya shabiki wa Yanga na Simba au timu nyingine? Au ndiyo ule mtindo
kwamba mtu anapokuwa katika kundi la watu anataka kuwaonyesha yeye ni hatari
sana akikasirika na anaweza kung’oa viti.
Kama hali hiyo itaendelea mwisho wake nini au anayefanya vile
anafaidika nini? Kwanini kama mashabiki wanazozana au kugombana, basi wasifanye
hivyo bila ya kugusa viti? Wanajua wanaingiza hasara kiasi gani kila
wanapofanya hivyo?
Mkatika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga dhidi
ya mabingwa Al Ahly, mashabiki wa Yanga na Simba walipigana mara kadhaa. Kila
hasira ziliyempanda alitumia viti vya uwanja huo kama silaha ya kupoteza hasira
zake au kumuumiza mpinzani wake.
Wakati fulani nilimshuhudia shabiki mmoja wa Simba, akijaribu
kumzuia shabiki mwenzake asirushe kiti alichokuwa nacho mkononi kwenda upande
wa mashabiki wa Yanga kwa kuwa akifanya hivyo, wale wa Yanga nao wangejibu
wakati yeye alikuwa na mtoto mdogo.
Hatari ya yule mtoto kuumizwa lakini ni dalili ya kusababisha
dada na mama zetu wahofie kwenda uwanjani sababu ya wapuuzi wachache wanaoamini
ni mashabiki wa kweli wa mpira, kumbe ni waharibifu na wahujumu uchumi
wanaotaka kuturudisha nyuma. P
ia nilimuona shabiki wa Simba akiwa amelazimika kuangalia
mpira huku akiwa amejifunika na kiti kichwani na kilichokuwa kimeng’olewa. Hofu
yake ilikuwa ni hivi, wakati anaangalia mpira, kiti kinaweza kuvurumishwa
kutoka upande wa Yanga na kikatua kichwani mwake.
Ushabiki wa kishamba, ushabiki wa kizamani, watu wa kizamani
na wenye mawazo hasi yasiyokuwa na gia songa. Wanataka Tanzania ibaki ileile
yenye viwanja ambavyo mashabiki wamekuwa wakikaa chini. Si vizuri, lakini
wanaweza kujipima hivi; wale wanyama ambao unawawekea chakula kwenye sahani,
wao wanatoa na kulia chini.
Watu wa usalama bado hawajawa wakali vya kutosha, kuna kila
sababu ya kuongeza nguvu na kuwamaliza watu wa namna hiyo. Sheria ichukue
mkondo wake, wanaonyesha akili zao zinashindwa kutambua kuwa matumizi ya viti
ni yapi. Basi hakuna haja ya kuwafundisha na badala yake adhabu iwakute.
Washughulikie, ikiwezekana mmoja au watakaopatikana na hatia
wafikishwe kizimbani kwa upuuzi wanaofanya ili iwe mfano. Mkiendelea kuwaachia,
wataufanya uwanja huo uwe na gofu kwa kisingizio cha hasira. Kama kweli ni watu
waliokasirika na wanashindwa kujitambua katika kipindi hicho, mbona hawatoi
simu zao mifukoni wakawaponda mashabiki wanaowabugudhi. Watu hawa hawatufai
kwenye jamii yetu.
0 COMMENTS:
Post a Comment