Na Saleh
Ally
YANGA
imevunja mwiko dhidi ya Waarabu wa Misri, imewafunga Al Ahly katika kipindi
wakiwa mabingwa wa Afrika na kikosi namba moja kwa ubora barani Afrika.
Yanga wana
kila sababu ya kuamini kwamba wana kikosi bora, si kwa bao moja pekee la Nadir
Haroub ‘Cannavaro’ lakini namna walivyocheza na kuwapa kazi kubwa Waarabu hao
wabishi.
Katika
mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyopigwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam, Yanga walionyesha uwezo wa juu lakini wakawa na kasoro
kadhaa, moja kubwa ni ile ya kutotumia nafasi walizozipata.
Wakati
Yanga inafungwa bao 1-0 na Al Ahly kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar mwaka
2009, kosa kama hilo pia lilitokea. Pamoja na kwamba walifungwa, lakini
walipoteza nafasi nyingi sana za kufunga kupitia Davies Mwape na Kenneth
Asamoah.
Walipokwenda
jijini Cairo, wakakutana na kipigo cha mabao 3-0, wakawa wametolewa kwa jumla
ya mabao 4-0, rekodi ya kuendelea kunyanyaswa na Waarabu ikaendelea kujazwa
uzito.
Sasa Yanga
wameivunja, wamewafunga Waarabu hao wenye uwezo mkubwa kisoka. Huo ni mwanzo,
hakuna anayejua kuwa kazi ni ngumu na ili Yanga iweke rekodi sahihi, lazima
ibaki njia kuu, ikichepuka tu, imekwisha!
Kusherehekea
ushindi wa bao 1-0 Taifa juzi ni sahihi kabisa. Lakini vizuri sherehe zisizidi
saa 24, badala yake maandalizi ya mechi ya mwisho inayotarajiwa kupigwa
Jumapili ijayo ndiyo yapewe nafasi kubwa hasa kwa kikosi cha Yanga.
Al Ahly
wameondoka, wakitua kwao moja kwa moja wataanza maandalizi na inawezekana
kabisa yatakuwa ni maandalizi ya juu kuliko walivyotarajia kwa kuwa wamepoteza
mchezo, kitu ambacho hawakutarajia.
Kocha Hans
van Der Pluijm amesema anajua kuwa fitna zitachukua nafasi kubwa, hilo
amejiandaa lakini uwezo wa soka, kila aliyekwenda uwanjani ameona, wanao, tena
ni mkubwa. Kama wakijumlisha na fitna, itakuwa ni kazi kubwa zaidi kwa Yanga.
Ili Yanga
ibaki njia kuu, lazima hesabu zake ziwe na muendelezo badala ya kuchepuka na
kuanza upya. Hadi walipofikia ni nusu ya safari, kama ingekuwa ni ligi ndiyo
mzunguko wa kwanza umemalizika na inajulikana wa pili unavyokuwa mgumu.
Muendelezo
ni muhimu, hadi kufikia walipo na kuifunga Al Ahly kwa mara ya kwanza nyumbani,
nini kilifanyika. Lakini sasa ni wakati mwafaka wa kuingia B kwa kutumia A
ambayo ni muhimu sana kwao.
Kuingia
kwenye hatua ya pili kwa kufuata njia waliyoanzia bila ya kuchepuka kutajenga
muendelezo na kufanya Yanga iwe na nafasi ya kufanya vizuri Cairo.
Wanachotakiwa
kuamini ni kazi imefanyika nusu, nusu iliyobaki lazima ifanyiwe kazi kikamilivu
na kitu kizuri zaidi ya Yanga wamewaona Ahly wakipambana nao lakini lazima
wajue huo ni mchezo wa ugenini.
Vichwa:
Wachezaji
wa Ahly walizozana sana baada ya kufungwa, si kwamba pekee hawapendi kufungwa,
lakini kilichowaudhi ni bao la kichwa. Kwamba wao ni warefu na wana uwezo wa
kupiga zaidi mipira ya juu.
Walilia na
uzembe wao na kweli ndiyo uliosababisha wao kufungwa. Utaona kwa asilimia 70
mipira ya juu ilikuwa yao na si kwa wachezaji wa Yanga.
Kwa hili,
Yanga lazima wajue kuna kazi ya kufanya, Ahly walipata shida na mipira ya
chini, Yanga kuinua juu mipira ni sawa na kuigawa sadaka.
Mashuti:
Kingine
ambacho kilionekana ni kosa kubwa kwa Yanga, ni wachezaji wake kurudi nyuma
wakati wa kukaba na kuruhusu Waarabu hao kukimbia hadi zaidi ya mita 10 na
mpira, halafu wakapiga mashuti.
Hakuna
ubishi wana nguvu na kama mashuti yao yakilenga lango, basi ni hatari. Iwe
isiwe, lazima Yanga walifanyie kazi suala hilo. La sivyo litakuwa tatizo kubwa.
Mabeki:
Walinzi wa
pembeni wa Yanga lazima wajue wao ni nusu ya uhai wa Yanga, utaona Ahly
walikuwa wakipambana kupata krosi. Inaonekana mfumo wa Pluijm uliwazima kufanya
walichotaka kwa asilimia kubwa.
Lakini
wakiwa Cairo haitakuwa kazi rahisi sana, lazima watapiga krosi nyingi na
wanategemea mipira mingi ya vichwa, wana sifa ya kuwa wazuri kwenye kufunga
mabao ya vichwa, pia wana miili mikubwa, hivyo wana nafasi ya kufunga.
Kama mabeki
wa pembeni watacheza kwa uwezo wa juu, mawinga au viungo watawasaidia kukaba na
kuziba mifereji ya krosi, watasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza hatari.
Kujiamini:
Huenda
wengi hawakuliona hili, ila kuna wachezaji wa Yanga walikuwa na ‘mcheche’, hata
kutoa pasi ilikuwa shida. Hapo ni nyumbani, kama wakifanya hivyo ugenini
litakuwa ni tatizo kubwa. Hivyo lazima wajiamini na kuonyesha uwezo kwa kufuata
mipango ya kocha.
Haya ni
machache, kocha na benchi la ufundi la Yanga linajua mengi zaidi. Kikubwa hapa
ni kubaki njia kuu na kuendeleza kufanya mambo kwa uhakika, kikubwa wakumbuke,
mechi ijayo itakuwa ngumu zaidi ya ile ya juzi Taifa.
0 COMMENTS:
Post a Comment