UMESIKIA
mzozo uliopo kati ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) na Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF)? Watu hao
hawaelewani na sasa kuna hata baadhi ya viongozi hawazungumzi vizuri!
Mfarakano
huo upo ingawa kila upande unajaribu kuficha kutaka ionekane mambo yako safi,
lakini si kweli. Katika uchunguzi wangu wa takribani wiki inaonekana karibu
kila upande kuna tatizo lakini suala la fedha ndiyo limezaaa yote hayo.
Fedha
inaonekana kuwa chanzo cha mgogoro huo na sasa kumekuwa na taarifa kuwa TFF
imekuwa kwenye mchakato wa kuivunja bodi ya ligi ili ishike tena hatamu ya
kiongoza Ligi Kuu Bara na mamilioni yaendelee kuingia kwenye shirikisho hilo
kama ilivyokuwa awali.
Stori ziko
nyingi kila upande, katika gazeti hili juzi, Rais wa TFF, Jamal Malinzi
alihojiwa na kusema hafahamu lolote kuhusiana na suala hilo. Lakini upande wa
bodi wakaeleza kumekuwa na kulazimisha matumizi mabaya ya fedha.
Kwamba kuna
viongozi wa TFF wamekuwa wakitaka fedha zitoke kiholela na wakati mwingine
wapewe watu fulani-fulani. Upande huo ukaendelea kufafanua kuwa TFF imewatuhumu
kutumia fedha za baadhi ya timu zilizotolewa na wadhamini.
Lakini wao
bodi wakawaambia hawakuwa na malalamiko ya klabu yoyote kutopewa au kucheleweshewa
fedha zake, lakini TFF ikaamua kupeleka mkaguzi wa mahesabu ambaye hakuwa
akifanya kazi za TFF kama kanuni zinavyoeleza, wao wakamkataa na kusisitiza
watakaguliwa na mkaguzi wa shirikisho na si yule binafsi aliyeletwa tu na mmoja
wa viongozi.
Hilo nalo
likawa ni chanzo cha mgogoro huo unaoendelea na TFF wakasema kuwa bodi hawataki
kukaguliwa, hali ambayo inasababisha kuwepo na walakini wa mambo. Ndiyo maana
nimeanza na kusema huenda kila upande una tatizo.
Lakini kama
kweli ina mpango wa kuivunja bodi hiyo na chanzo kinaonekana ni masuala ya
fedha, basi hicho kitakuwa ni kichekesho cha aina yake kupitia mambo mawili.
Nitafafanua.
Kwanza,
baadhi ya viongozi wa TFF kabla ya kuingia madarakani, wakati huo chini ya
uongozi wa Leodegar Chilla Tenga, walikuwa wakifanya kila juhudi, walisaidia
kuhakikisha kamati hiyo ya bodi inaundwa na uendeshaji ligi unaondoka mikononi
mwa Tenga na TFF yake. Sasa vipi leo waone tena bodi ya ligi haifai?
Pili, kama
TFF na bodi ya ligi ndiyo wanaopaswa kushirikiana kuhakikisha ligi hiyo
inapanda kiwango na ikiwezekana kuchangia kuhamisisha soka nchini kuanzia chini
hadi juu, vipi wao ndiyo waanze kufarakana mapema na tena kisa ni fedha?
Kama ni
maendeleo ya soka, basi TFF na bodi ya ligi wana safari ndefu sana ya kwenda kuhakikisha
mpira wetu unaendelea. Kama mapema hivi wameanza kulumbana, basi maana ya
kuanzishwa kwa bodi hiyo itapotea kabisa, badala yake itakuwa ni sawa na
kuanzisha chombo kingine cha migogoro na mwisho itakuwa ni hasara tu kwa mpira
wa Tanzania, maana mtakuwa mnachochea kuni za kuumaliza mpira wetu kabisa.
Bado
ninasisitiza, kuna wale washauri wa karibu wa viongozi wa juu wa TFF mnapaswa
kuwa makini, mtumie busara na mjue kuwa TFF si mahali kwa ajili ya kuchuma na
badala yake kujitolea zaidi kwa ajili ya kuleta maendeleo, kama hamuwezi, kaeni
kando.
Tumelalamika
sana kuhusiana na Tenga, lakini hakuna waliompongeza hata kwa machache mazuri
aliyoyafanya. Mlioingia mnapaswa kujifunza kwake lakini mkumbuke, kuongoza TFF
si kuchuma tu, badala yake kuleta maendeleo.
Ugomvi kwa
ajili ya fedha ni dalili ya kutoonyesha uaminifu, kuiua kamati ya ligi leo,
itakuwa ni kudhihirisha tamaa zenu au kuchota fedha haraka. Mimi ninaamini
huenda mlifikiri tu mnataka kufanya hivyo, lakini najua mtakuwa mmetafakari na
kuachana na mawazo hayo kwa kuwa kuna mambo mengi ya maendeleo ya kufanya
kuliko kuanzisha mjadala ‘tasa’ usiokuwa na sababu zozote za kuuanzisha.
0 COMMENTS:
Post a Comment