Na Saleh Ally
KOCHA anachukua nafasi ya mzazi katika kikosi chochote
cha soka, mara nyingi kama kunakuwa kuna mafanikio basi yanasherehekewa na kila
mmoja hadi mashabiki, lakini ikitokea mambo yameharibika, mzigo anabebeshwa
kocha.
Kulibadilisha hili katika hali ya kawaida ni vigumu
sana, unaweza kusema ni mazoea au ndiyo utamaduni katika soka. Lakini kwa nini
mafanikio mara zote hayaonekani ni kutokana na ujuzi wa kocha, badala yake kila
mmoja hugawiwa sifa na akiyumba, ubovu anaangushiwa yeye?
Kila timu inapofanya vibaya, lazima kocha anachukuliwa
hatua. Kuna mifano mingi lakini huenda kikosi cha Yanga kinaweza kuwa mfano
mzuri kujadili suala la namna makocha wanavyoangushiwa gunia la misumari kila
timu inapofanya vibaya.
Ernie Brandts, aliondolewa Yanga na ikaelezwa kuwa
alishindwa kudhibiti suala la nidhamu kutokana na kikosi chake kuwa na
wachezaji wengi wenye majina makubwa. Akatupiwa virago ili aondoke zake na
Yanga ianze kusaka kocha mpya.
Kabla ya kuondoka kurejea kwao Uholanzi, Brandts naye
akatupa lawama kibao kwa baadhi ya viongozi kuwa wamekuwa tatizo ndani ya Yanga
na wamechangia kuporomoka kwa nidhamu kwa kuwa wanajenga hisia za wachezaji
kumdharau yeye na watu wengi wa benchi la ufundi, hilo likapita.
Safari hii akaajiriwa Hans van Der Pluijm, pia raia wa
Uholanzi. Pamoja na kuwa na rekodi nzuri akiwa na kikosi cha Berekum Chelsea
cha Ghana, bado baadhi hawakukubaliana na ujio wake, huenda walimuona ni mtu
mzima sana, akapewa jina la ‘Babu’.
Siku zote si rahisi watu kukubali jambo moja. Lakini
ndani ya kipindi kifupi tu, van Der Pluijm alifanikiwa kufanya mabadiliko
makubwa kwenye kikosi cha Yanga hasa katika suala la uchezaji. Mpangilio na
makali yakaongezeka.
Yanga ikaonekana inatisha, katika michuano ya
kimataifa ikashinda idadi kuwa ya mabao dhidi ya Komorozine ya Comoro, ikaitoa
kwa jumla ya mabao 12-2. Ikasonga mbele ikakutana na Al Ahly, hawa ni mabingwa
wa Afrika na Misri. Ikawafunga bao 1-0 jijini Dar na kuandika rekodi mpya.
Imani Yanga ingefanya vizuri katika mchezo wa
marudiano ilikuwa kubwa, kweli ilifungwa bao moja. Ikawa zamu ya mikwaju ya
penalti, Yanga ikatolewa kwa mikwaju 4-3. Funzo linaanzia hapo, hadi katika
mechi mbili za ligi tangu irejee kutokea Misri.
Mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara ni dhidi ya Mtibwa
mjini Morogoro, matokeo ilikuwa suluhu. Juzi ilirejea jijini na kutoka sare ya
bao 1-1 dhidi ya Azam FC ambao ndiyo vinara wa ligi hiyo.
Kama uliona mechi dhidi ya Al Ahly Dar na ile ya
Alexandria, halafu mechi mbili dhidi ya Mtibwa na ile ya Azam, juzi, utakubali
kuwa Yanga ilistahili kushinda. Swali, kwa nini haikushinda?
Siku chache zijazo utasikia van Der Pluijm na benchi
lake la ufundi wanaonekana hawana kitu, lakini cha kujiuliza, tatizo ni wao au
wachezaji! Kwa kuwa Yanga sasa ina sifa ya kupoteza nafasi, je, kuna sababu ya
kuamini yale maneno ya Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic au van Der Pluijm kwa
wachezaji wa hapa nyumbani na ukanda wetu wana tatizo la viwango bora?
Au tuamini maneno ya mchambuzi wa masuala ya soka ya
Afrika Magharibi kutoka runinga ya michezo ya Super Sport, Mamadou Gaye kuwa
wachezaji wengi wa ukanda wetu hawana nidhamu ya mchezo na wamekuwa wakiwaponza
makocha wengi?
Angalia nafasi walizozipoteza Yanga katika mechi ya
kwanza dhidi ya Al Ahly, zinazidi nne, wakafunga bao moja na likachangia wao
kutolewa.
Walipokwenda Misri, nakukumbusha nafasi mbili tu ndani
ya dakika 90, ile ya Simon Msuva timu zote zikiwa hazijapata bao na nyingine ya
Frank Domayo, Yanga ikiwa nyuma kwa bao moja.
Wakati wa mikwaju ya penalti, ingawa mashabiki wengi
walimlaumu Said Bahanuzi, lakini waliopoteza nafasi ni yeye, Oscar Joshua na
Mbuyu Twite aliyepiga penalti ya mwisho ya Yanga na alipokosa akaitumbukiza
shimoni, ikatolewa.
Ukirudi mechi mbili za Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa,
nafasi za Emmanuel Okwi, Didier Kavumbagu na wenzake zote hazikuhitaji bahati
mbaya, ilikuwa ni lazima kuzitumia ili timu yao ishinde.
Mechi ya juzi, kila aliyeiona uwanjani au kwenye
runinga anakubali Yanga ilistahili kushinda lakini kilichowaangusha ni kuchezea
nafasi za wazi, ukiwamo mkwaju wa penalti wa Hamisi Kiiza.
Mambo ni rahisi tu kwa mchezaji akiishasema: “I am
very sorry”, yaani samahani. Kwisha kazi na mashabiki, viongozi na hata
wachezaji wenyewe watasahau ndani ya siku mbili kwa kila kitakachotokea.
Mwisho huenda mzigo ukamuangukia Pluijm na benchi lake
la ufundi. Je, kuna atakayekuwa anakumbuka kwamba wachezaji kutokuwa makini na
kutimiza kazi yao vizuri ni tatizo pia?
Unaamini kumbadili kocha wakati wachezaji wakiendelea
kutokuwa makini ni sahihi au ndiyo kumaliza tatizo lenyewe? Jibu litakuwa
hapana, lakini kinachofanyika ni kufanya kazi kwa mazoea.
Mfano wa Yanga unaweza kuwa mzuri zaidi kutokana na
mambo kujipanga vema kuweza kuyazungumzia. Lakini hali hii inatokea Simba kwa
Logarusic na kwingine kwa makocha wengine, mfano Mtibwa, Kagera Sugar, Ashanti
United, Coastal Union na kwingineko.
Huenda hata wachezaji wanapaswa kujitathmini, kwamba
wanatekeleza kazi yao kwa ubora wa kiasi kipi?
Au wanafanya hivyo kwa kuwa siku ya uamuzi, mzigo au
gunia la misumari litabaki kwa kocha? Iko haja ya kubadili mfumo wa
uwajibishaji na kuangalia tatizo linapoanzia. Kocha anapotoa maelekezo ya
uhakika, suala la kuutumbukiza mpira wavuni linabaki kuwa la mchezaji. Naye
anapaswa kuwajibika ili kuepusha kumtumia mwalimu gunia ya misumari, pia
nidhamu ya mchezo idumishwe.
Hii inawahusu wachezaji wote wa Ligi Kuu Bara, Ligi
Daraja la Kwanza na iwe kwa wenyeji na wageni, bila ya kujali timu ipi.
0 COMMENTS:
Post a Comment