March 7, 2014

YANGA BAADA YA KUWASILI, WAKIELEKEA KWENYE BASI WALILOTENGEWA NA UBALOZI PIA UONGOZI WAO.

Na Saleh Ally, Cairo
Iilikuwa ni kama filamu mara tu baada ya Yanga kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Cairo jijini hapa, mambo yakawa kama kuna mkutano wa siasa.

YANGA WAKIINGIA KWENYE BASI

Idadi kubwa ya waandishi wa habari ilikuwa uwanjani hapo wakitaka kujua kila jambo, lakini Yanga pia wakakataa basi walilokuwa wameletewa na wenyeji wao Al Ahly na kupanda lile lililoandaliwa na ubalizi wa Tanzania nchini hapa.
BASI WALILOLIKATAA YANGA LIKIONDOKA UWANJA WA NDEGE WA CAIRO

Ndege ya Egypt Air iliwasili saa 12:05 kwa saa za hapa, ikiwa ni saa moja nyuma nyumbani na mara baada ya wachezaji kutoka, waandishi walianza kuwazonga wakiwakimbiza kutaka kupata mahojiano.
Wachezaji wa Yanga walikuwa kimya, hakuna aliyezungumza na badala yake wote walifululiza hadi kuingia kwenye basi hilo walilotengewa na ubalozi.

Wakati wote huo, Balozi wa Tanzania nchini Misri, Mohammed Haji Hamza na maofisa wake alikuwa uwanjani hapo akihakikisha mambo yote yanakwenda vizuri na katika mpangilio unaotakiwa.
Baadaye alizungumza na waandishi na kuwataka wavute subira kwa kuwa ndiyo timu ilikuwa imefika na hakukuwa na sababu ya papara hata kidogo.
“Sasa ndiyo timu imefika, nafikiri kuna mambo mengi tunapaswa kufanya kiutaratibu, hivyo mgetuacha kidogo halafu baadaye tutazungumza. Lakini vijana wamefika salama kama mlivyowaona,” alisema balozi huyo ambaye ofisi yake imetoa ushirikiano mkubwa kwa Yanga. 

Lakini tayari walishaelezwa kutozungumza lolote na moja kwa moja kwa kufuata maelekezo ya maofisa wa ubalozi wa Tanzania, wachezaji waliingia kwenye basi na kumuacha mwalimu, Hans van Der Pluijm akizungumza na waandishi hao.

Kabla ya hapo, waandishi hao walitaka kujua mengi hata kabla ya timu kufika, lakini msemaji wa Yanga, Baraka Kizuguto aliyekuwa jijini hapa takribani siku nne akautupia mzigo huo kwa balozi wa Tanzania nchini hapa, Mohammed Haji Hamza.

Yanga waliingia kwenye basi hilo aina ya Yutong na kuachana na lile aina ya Mercedes Benz walilokuwa wamepelekewa na Al Ahly.
Hali hiyo ilizua mshangao mkubwa kwa waliokuwa wameleta basi hilo, lakini Yanga wakasisitiza kwamba watapanda basi hilo.

Juhudi za waandishi hao wa Cairo kutaka kujua Yanga wanafikia wapi ziligonga mwamba na wakaelezwa timu itakwenda ubalozini.
Yanga iliondoka eneo la uwanja wa ndege na msafara wa basin a king’ora cha Polisi, lakini ajabu kilibaki nyuma wakati basi lilianza kuondoka.

Basi lenye rangi ya bluu lililoletwa na Al Ahly uwanjani pale, nalo liliondoka likiwa na dereva tu huku mmoja wa wahusika akionekana kukerwa na jambo hilo.
SOURCE: CHAMPIONI NEWSPAPER

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic