TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Nimepokea kwa masikitiko makubwa habari zilizotolewa na uongozi
wa Coastal Union kupitia Mwenyekiti wake, Ahmed Aurora katika gazeti la
Mwananchi la tarehe 23/04/2014 kwamba kwa kipindi cha miaka minne ambacho jina
la kampuni yangu limekuwa likihusishwa na jezi za Coastal Union, sijatoa kiasi
chochote cha pesa kulipia tangazo hilo.
Ukweli ni kwamba, ingawa hakukuwa na mkataba wowote wa maandishi
baina ya Binslum Tyres Limited, lakini mchango wangu kipesa katika klabu ya
Coastal umekuwa mkubwa na wa gharama kubwa kuliko kama ningeingia mkataba
na Coastal Union.
Niliigharamia Coastal Union kama Mwanachama, mnazi na shabiki wa
klabu hii bila ya kujali misingi ya kiudhamini kwa kipindi cha miaka minne.
Nimetumia zaidi ya shilingi 300 milioni kwa shughuli mbalimbali za klabu hii na
mashabiki wa timu hii na viongozi wanaoweza kusutwa na nafsi zao ni mashahidi
wakubwa katika hili.
Nimetumia zaidi ya shilingi 200 milioni kwa ajili ya kusajili
wachezaji pekee. Wachezaji hawa ni wale wenye majina makubwa na madogo ambao
wakati mwingine nililazimika mwenyewe kusafiri kwenda kuwanunua nchini jirani
kama Jerry Santo na Crispian Odula ambao nililazimika kusafiri mpaka Kenya
kwenda kuwanunua.
Nimetumia zaidi ya shilingi 100 milioni kwa ajili ya kugharamia
mishahara, posho na bonasi za wachezaji, mshahara wa kocha kama Hemed Morocco
kwa mwaka mzima, na baadhi ya maofisa wa timu. nimeandaa kambi zote za timu
tangu ilipopanda Ligi Kuu pamoja na kugharamia safari za timu katika mikoa
mbalimbali.
Sijawahi kuwa na nia ya kuvitaja vitu hivi hadharani, lakini
inapofika mahali ambapo mtu mzito katika klabu kama Mwenyekiti anaongea na
vyombo vya habari kupotosha ukweli huu, nalazimika kulinda heshima yangu
binafsi, heshima ya familia, na heshima ya kampuni ambayo nimeihasisi kwa jasho
kubwa kwa msaada wote wa Mwenyezi Mungu.
Lengo langu halijawahi kuitangaza Kampuni yangu kupitia jezi za
Coastal Union. Lengo langu lilikuwa kuipa hadhi jezi ya Coastal na kuongeza
ushindani kwa makampuni kuwania kutangaza bidhaa zao kupitia jezi za Coastal.
Kama ningeamua kuitangaza kampuni ya Binslum katika jezi ya
Coastal kibiashara, ningeweza kutumia hata shilingi milioni 50 tu ndani ya
kipindi cha miaka minne kwa sababu nina uhakika wasingekataa. Kwa sasa Coastal
bado haipo katika hadhi ya kudhaminiwa kwa mabilioni ya pesa kama Simba na
Yanga.
Vinginevyo ningeweza kuzidhamini klabu za Simba, Yanga, Mtibwa
Sugar, Tanzania Prisons, JKT Ruvu na nyingine ambazo ziliendelea kuwepo Ligi
Kuu ya Tanzania Bara hata wakati Coastal ikiwa madaraja ya chini.
Niliamua kuingiza pesa nyingi Coastal Union kama shabiki, mnazi
na mkereketwa na sitarajii pesa hizo kurudi katika faida ya kampuni kwa sababu
Coastal Union sio njia kuu ya utangazaji wa bidhaa za Binslum kuliko Magazeti,
Televisheni na redio na matangazo ya barabarani.
Ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba nimepokea kwa masikitiko
makubwa taarifa ya Bwana Aurora, ingawa nitaendelea kuwa shabiki na mwanachama
mkubwa wa Coastal Union ambayo nimeishabikia tangu utotoni.
Nimeamua kuweka bayana ukweli huu na kwa sababu Mungu ameyaona
yote niliyoyatenda Coastal Union, yeye ndiye atakayekuwa shahidi wangu katika
hili.
Nassor Binslum
Managing Director
Binslum
Tyres Limited
0 COMMENTS:
Post a Comment