Mambo bado ni
magumu mkoani Shinyanga, uongozi wa timu ya soka ya Mwadui ya mkoani humo,
umedai kuwa upo tayari kutumia mamilioni ya fedha mpaka makao makuu ya
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ili kuhakikisha unapata haki yake ya
kushiriki ligi kuu msimu ujao, kama Rais wa TFF, Jamal Malinzi alivyofanya
wakati anataka uongozi huo.
TFF wameitangaza
Stand kuwa ndiyo imepanda daraja baada ya kushinda rufaa yake na kupewa pointi
tatu za mezani kutokana na madai ya Kanembwa kuchezesha wachezaji waliosajiliwa
wakati wa dirisha dogo kwenye mechi yao ya mzunguko wa kwanza iliyorudiwa.
Hali hiyo
imewaweka katika wakati mgumu viongozi wa Mwadui ambao walikuwa na matumaini
makubwa ya kuiona timu yao hiyo ikishiriki michuano ya ligi kuu msimu ujao.
Kocha Mkuu wa Mwadui, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, alisema
uongozi wa timu hiyo umejipanga kuhakikisha haki yao inapatikana kwa gharama
yoyote ile.
Alisema
wanatarajia kuwasilisha rufaa yao TFF, muda wowote kuanzia sasa ili kupinga
uamuzi wa shirikisho hilo kuizawadia Stand United pointi tatu za mezani na kama
litashindwa kuwapa haki yao, basi watatinga Fifa.
“Tunatarajia
kupeleka TFF rufaa yetu muda wowote kuanzia sasa ili kudai haki yetu kwani
hatupo tayari kuona inapotea hivihivi kwa sababu ya maslahi ya watu wachache.
“Tutafuata
taratibu zote mpaka kuhakikisha inapatikana na ikiwezekana tutafika Fifa ili
kuipata kama alivyofanya Malinzi alipokuwa akitaka kuingia TFF, uongozi wetu
umesema kuwa upo tayari kwa jambo hilo na umejipanga kwa kila kitu ili
kuhakikisha tunapata haki yetu hiyo,” alisema Julio.
Pointi moja tu
ndiyo iliyoinyima Mwadui tiketi ya kushiriki ligi kuu msimu ujao ambapo kabla
ya Stand United kupewa ponti tatu za mezani, Mwadui ilikuwa ikiongoza kundi
lake kwa pointi 31 na Stand United ilikuwa ya pili (pointi 29).
0 COMMENTS:
Post a Comment