Na Saleh
Ally
LIGI Kuu
Bara msimu wa 2013-14 imefikia tamati kwa Azam FC kuweka rekodi mpya ya kuwa
moja ya timu ambazo si Yanga wala Simba ambazo zimewahi kutwaa ubingwa wa ligi
hiyo.
Walichokifanya
Azam FC ni moja ya rekodi ambazo zinaweza kuwa na hamasa ya kuongeza tamaa na
hali ya kujiamini kwa timu nyingine kwamba soka linaweza kuwa la ushindani
zaidi nchini na wanaoweza kupata ubingwa au mafanikio si Yanga au Simba pekee.
Lakini
wakati ligi imemalizika, burudani ilikuwa ni ile mechi ya watani wa jadi Simba
na Yanga ambao walikuwa wanafunga msimu na kama kawaida, wanapokutana inakuwa
ni burudani. Siku ya mechi hiyo iliyokuwa ni ya kufunga msimu, mshambuliaji
Amissi Tambwe wa Simba ambaye ameibuka kuwa mfungaji bora alituzwa.
TAMBWE KAZINI |
Tambwe raia
wa Burundi, alipokea tuzo yenye thamani ya Sh 50,000 tu ambayo amepewa kutokana
na uwezo aliouonyesha wa upachikaji mabao, kwani amefunga 19 na ndiye mfungaji
bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2013-14.
Mrundi huyo
hakupewa tuzo hiyo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wala wadhamini wa ligi
hiyo, Vodacom. Tuzo hiyo imetolewa na William Punde, mkazi wa Mburahati jijini
Dar es Salaam ambaye ni mlemavu lakini mpenda michezo na shabiki wa Simba.
Punde
alimkabidhi Tambwe tuzo aliyoitengeneza kwa gharama ya Sh 50,000 huku akisema
kama angeiuza, basi angepata kuanzia Sh 150,000 hadi 200,000. Lakini aliona
amzawadie Tambwe na kama haitoshi ana zawadi kwa ajili ya mabingwa wapya, Azam
FC.
Shabiki
huyo wa Simba ni fundi seremala katika kampuni ya Auto Make maeneo ya Tabata
jijini Dar es Salaam na anavutiwa zaidi na kazi ya sanaa ndiyo maana aliamua
kutumia fedha yake kuchonga zawadi hiyo kwa Tambwe akiamini kukubali kazi za
watu ni jambo jema.
Punde baba
wa watoto wawili, Jesca William (16) na Frank William (10) ambao amewapata
akiwa na mkewe Lucy Mathayo, amekuwa akishiriki kwenye mambo ya michezo kupitia
‘chama’ lake la Milambo la Mburahati, lakini kuna timu ya watoto ya Mburahati
United.
Kwa nini
Tambwe?
Niliamua
kumpa tuzo Tambwe kwa kuwa amefanya kazi kubwa, ameonyesha uwezo na kweli
alistahili kwa kuwa amejituma. Anayefanya vizuri ni mtu ambaye anatakiwa
kupongezwa kutokana na alichokifanya, huo ndiyo ulikuwa uamuzi wangu.
Unafaidika?
Faida ni
kuridhisha nafsi yangu, lakini pia kutoa somo kwamba hata mimi, licha ya kuwa
mlemavu bado ninaweza kusaidia na si kusaidiwa tu. Pia ninaweza kuwa nina
mchango wangu pamoja na kwamba sina kipato kikubwa lakini lengo ni kuonyesha
mapenzi na nia yangu ya kukuza kitu.
Tuzo:
Niliamua kutengeneza
tuzo hiyo yenye mfumo wa kiatu pamoja na mpira kwa kuwa nimeona baadhi ya tuzo
kubwa duniani. Niliitengeneza kwa siku kadhaa na pia nilifanya kwa umakini
mkubwa kwa kuwa ninaamini itanitangaza.
Watu
kukubali kazi zako inachukua muda, lakini ubora unaweza kukufanya ukubalike.
Mimi ni shabiki wa Simba, hivyo nilimtengenezea tuzo Tambwe kwanza
kanifurahisha, lakini pia mchango wake kama nilivyosema. Pia niliangalia ubora
kwa lengo la kujitangaza kikazi.
Hii si mara
yangu ya kwanza kutoa tuzo kwa mtu au watu, nimekuwa nikifanya hivyo. Nakumbuka
mwaka 2010, nilimtengenezea tuzo msanii Mrisho Mpoto na nilikuwa ninampongeza
kuanzisha mashindano ya mashairi na mwanangu pia ni msanii mzuri sana.
Ubora:
Naweza
kutengeneza tuzo yenye ubora zaidi ya hapo, lakini inategemea na vifaa
ninavyotumia. Unajua ubora zaidi wa vifaa unaongeza kitu kuwa na thamani zaidi.
Sasa mimi pia inategemea na kipato changu, lakini ninachoweza kukuhakikishia ni
kwamba ninatengeneza vifaa ambavyo ni bora.
Ulemavu:
Kweli kuna
wale walemavu wanaamini sisi ni watu wa kusaidiwa tu, inapobidi si vibaya.
Lakini kujiamini ni kitu bora sana kwa kuwa tunaweza kufanya mambo makubwa.
Nayakumbuka sana majina ya (Reginald) Mengi ambaye amekuwa akitueleza kwamba
tujiamini kwa kile kiungo ambacho kinafanya kazi na kukitumia.
Hivyo mimi
ninajua nina viungo vipi viko kamili na vinaweza kunisaidia na kufanya mambo
makubwa. Ninajiamini ninaweza kufanya mambo makubwa ndiyo maana nimekuwa si
muoga na ninataka kufanya mambo ambayo huenda yatawashangaza wengi licha ya
kwamba bado kipato changu hakipo juu.
Punde
anasema ataendelea kusaidia kila atakapoona anaweza kufanya hivyo kwa lengo la
kutimiza nia na mapenzi yake. Lakini baadaye anataka kuwa msanii wa kimataifa
ambaye ikiwezekana atakuwa akichonga tuzo kubwa-kubwa ambazo watapewa wachezaji
nyota kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika na ikiwezekana dunia nzima.
0 COMMENTS:
Post a Comment