Na Saleh Ally
KOCHA Jamhuri
Kihwelo ‘Julio’ ni kati ya wadau wakubwa na sehemu ya sura ya mchezo wa soka
hapa nyumbani, ataendelea kuwa gumzo kwa miaka mingi ijayo bila ya kujali yu
hai au la.
Julio ni kati ya
wachezaji wachache wa Tanzania ambao wamekuwa na mwendelezo mzuri tokea wakiwa
wachezaji hadi walipofikia kuchukua nafasi ya ukocha.
Beki huyo wa
zamani wa Simba, amekuwa na mafanikio wakati akicheza lakini ameendelea kufanya
hivyo baada ya kuanza kufanya kazi katika nafasi ya ukocha.
Moja ya sifa
kubwa ya Julio ni ucheshi, maneno ya vichekesho na hata yale ya shombo ili mradi
inategemea ni wakati gani. Ni kivutio kwa wadau wa soka na amekuwa akizidi
kuongeza chachu ya burudani ya mchezo huo.
Mimi binafsi
kupitia Championi, nimekuwa nikimkosoa Julio mara kadhaa kutokana na mambo
mbalimbali ambayo yalitokea akiwa kocha wa Simba kwa vipindi tofauti.
Najua nitakuwa
ninamuudhi sana, lakini sijawahi kulifikiria hilo sana kwa kuwa ninapomkosoa,
zaidi huwa ninalenda kurekebisha kwa manufaa ya mpira wa Tanzania na si
vinginevyo.
Lakini
inapofikia wakati wa kusifia, basi ni kipindi kizuri kumpa mtu sifa ya kile
ambacho amekifanya kama ambavyo alivyofanya kocha huyo akiwa na timu yake ya
Mwadui United ya mkoani Shinyanga.
Mwadui United
iliyokuwa inaongozwa na Julio imepambana hadi kufikia kupanda daraja, yaani
Ligi Kuu Bara na kuwaacha jirani zao Stand United kwa muda tu, kwani wakati
Mwadui wakisherekea kupanda daraja, taarifa za Stand kushinda rufaa yao dhidi
ya Kanembwa ziliwadia na kuwapa nafasi ya kupanda.
Unaweza kusema
kwa mara nyingine, Julio alichungulia Ligi Kuu Bara kwa sekunde kadhaa tu na
baada ya hapo akarejea tena Ligi Daraja la Kwanza, ndiyo maana amekuwa na jazba
kuhusiana na suala la Stand United kupanda.
Julio ana haki
kama walivyo na haki Stand ambao walikuwa wamekata rufaa. Kwa kuwa ni kocha,
ukaachana na rufaa utaona Julio ni kocha aliyeipandisha timu ligi kuu na hilo
halina ubishi. Jiulize, timu aliyoipandisha ni ipi?
Julio aliamua
kujiunga na Mwadui ambayo iko mkoani Shinyanga, tena si mjini, mwendo wa
takribani dakika 45 kutoka Shinyanga mjini. Kipindi hicho ndiyo alikuwa
ametemwa Simba.
Kwa kocha ambaye
haiamini kazi yake, haraka asingekubali kwenda kwenye timu ambayo haina jina na
inawania kucheza Ligi Kuu Bara. Lakini Julio akafanya hivyo, tena katika
kipindi kigumu na somo langu la leo linaanzia hapo.
Hii inaonyesha
Julio pamoja na kusifika kwa ‘mdomo mwingi’, lakini si mtu wa maneno tu, badala
yake anaiamini kazi yake, anaamini anachokifanya, ndiyo maana alijiamini kwenda
Shinyanga na kuifundisha Mwadui ambayo ilikuwa na jina kubwa enzi zile akina Julio
wanacheza.
Julio anatokea
katika familia ya soka, lakini hicho hakiwezi kuwa kigezo cha cha ubora wake,
kwani hata wadogo zake walikuwa wanasoka mahiri lakini hawajafikia alipo, hii
inaonyesha ana kipaji na anajituma kufikia alipo.
Inawezekana
ikawa ni rahisi kumdharau Julio kwa kuwa ana maneno mengi, au kwa vile
alishafukuzwa Simba halafu akarudi kila inapotokea ameitwa tena. Ukweli ni
kwamba ni kocha mzalendo anayeiweza kazi yake, tofauti zake za kibinadamu weka
kando.
Kupongezana ni
jambo jema. Shikamoo Julio, natoa saluti kwa kazi yako safari hii na
ikiwezekana unaweza kufanya vizuri zaidi ya ulivyofanya sasa kama utaendelea
kujiamini lakini ukakaa kwenye mstari sahihi ambao unaamini utakusaidia kukua
na kukuza mpira wetu.
Kwenye soka sasa
Julio ni baba, ingawa watoto wako Super na kaka yake tayari wanacheza soka nje
ya Tanzania, lakini misingi bora inatakiwa kwenye soka hapa nyumbani na watu
wanaoweza kuwa mfano ni wewe na watu wa aina yako walio tayari kujitolea.
Tabia ya ukweli
ni sehemu kubwa ya maendeleo katika kitu chochote duniani hata kama utakuwa
unawaumiza watu. Mara nyingi umekuwa mkweli, endelea hivyo kwa kuwa mara nyingi
umekuwa ukisema ukweli.
Ushauri mdogo
tu, vizuri ukapunguza jazba kwa kuwa penye wengi kuna mengi na hamuwezi kufanana
mnavyofikiria iwe ni sahihi au la! Mfano, siku ukitoka nje ya reli, basi
nitakuwa wa kwanza kukukosoa.
Makocha wengine
wazawa, mna mengi ya kujifunza kwa Julio, siwashauri mjifunze uongeaji, hicho
ni kipaji chake. Lakini uwezo wake wa kujenga kikosi, kuwashawishi vijana
kujituma na hali ya kujiamini aliyoionyesha kwenda kuichukua Mwadui na kuipa
mafanikio ni somo kubwa kwenu, msimuone ni mtu wa kubahatisha.
Kwanza mkubali
kwamba amefanya jambo zuri na lenye mafanikio, halafu pili tulieni mtadhimini
uzuri wake, baada ya hapo mjifunze na mtaona mtafaidika.
0 COMMENTS:
Post a Comment