April 12, 2014


Na Saleh Ally
LIGI Kuu Bara inakwenda ukingoni, timu zote 14, kila moja imebakiza mechi mbili mkononi ambazo zitatoa majibu mengi sana.
 Mechi hizo mbili kwa kila timu zina majibu mengi kwa kuwa kuna timu zinawania ubingwa na majibu yatapatikana kupitia mechi hizo, nyingine zinapambana kupata nafasi ya pili, hali kadhalika zile zinazokwenda kuteremka daraja.

Azam FC na Yanga ndiyo timu zenye nafasi ya kutwaa ubingwa ingawa Wana Lambalamba ndiyo wako katika nafasi nzuri zaidi. Mbeya City waliopanda msimu huu, wao wako katika mapambano ya kupata nafasi ya pili ili washiriki michuano ya Kombe la Shirikisho iliyo chini ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

Rhino wenye pointi 16, JKT Oljoro wenye 18, Prisons na Ashanti walio na pointi 22 kila mmoja pamoja na Mgambo walio na 25, anapambana kuepuka kuporomoka hadi Ligi Daraja la Kwanza Bara.

Lakini kuna timu zenyewe zipo tu, hazina ushindani wa lolote kwa kuwa haziwezi kupata lolote. Hazitateremka daraja, hazitashika nafasi ya pili, wala haziwezi kuwa bingwa na mojawapo ni Simba.
Simba ambayo imekuwa na heshima kubwa, sasa ina hofu hata ya kushika nafasi ya nne kwa kuwa pointi zake 37 zinaweza kufikiwa na Kagera Sugar yenye 33, kama itaboronga katika mechi mbili zilizobaki dhidi ya Ashanti United na Yanga.
Simba ya sasa, si ya zamani kwa kuwa ligi wakati inakwenda ukingoni inaonekana ni timu isiyowania lolote lile kwa maana si washindani kama ilivyozoeleka.
Msimu uliopita wa 2012-13, Simba ilishika nafasi ya tatu nyuma ya mabingwa Yanga na Azam FC walioshika nafasi ya pili. Msimu huu, zamu yao ni nafasi ya nne ikibidi ya tano ikizubaa, kitu ambacho kitakwimu kinaonyesha Simba inaendelea kuporomoka msimu hadi msimu.
Ndani ya msimu uliopita, kila nusu msimu ilifundishwa na makocha wawili, Milovan Cirkovic wa Serbia halafu Patrick Liewig raia wa Ufaransa, huo ulikuwa msimu wa 2012-13.
Msimu huu, makocha wawili pia. Mzunguko wa kwanza Abdallah Kibadeni ‘King Mputa’ na mzunguko wa pili, yuko Zdravko Logarusic raia wa Croatia. Hii inaonyesha kiasi gani mambo yanakwenda shaghalabaghala.
Tatizo kubwa kwa Simba linaonekana na jibu ni rahisi sana, kwamba kwenda vibaya kwa mambo ni tatizo la uongozi wa Simba yenyewe.
Kawaida wamekuwa wakikasirika, lakini inaonyesha kiasi gani Simba imeyumba kupita kiasi chini ya uongozi wa Ismail Aden Rage.
Kwa miaka miwili, Simba imekuwa timu ya kupigania heshima tu na wala si vikombe au kucheza michuano ya kimataifa. Maana yake, kama ingekuwa tena chini ya uongozi huo, msimu ujao ingepambana kupata nafasi ya sita au tano.
Hakuna kiongozi wa Simba anayeweza kulikwepa hilo, kwamba wameiporomosha, wameifanya iwe timu ya kawaida, isiyotisha kama lilivyo jina la Simba lakini ionekane si yenye mvuto kama ilivyokuwa misimu mitatu iliyopita.
Mashabiki na wanachama wa Simba wameliona hilo, hawana raha, ndiyo maana hawapendi hata kwenda uwanjani kuiona timu yao ikicheza kwa kuwa wanajua kwenda ni kuongeza maumivu mioyoni.
Wako wenye roho ngumu, wanakwenda na wanaendelea kujua makosa. Ndiyo maana inaweza kuwa wakati mwafaka kwao kwamba katika uchaguzi ujao wa uongozi, watalazimika kuchagua watu sahihi na si kubahatisha kama ilivyokuwa kwa uongozi wa Rage ambao unawatesa, unawaumiza na Simba si Simba tena!

TAKWIMU:
IMECHEZA     IMESHINDA    SARE    IMEPOTEZA
    24                       9                  10                5

INA  MABAO     IMEFUNGWA  MABAO          NAFASI
         40                             25                                 4




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic