Sasa yamemuelemea na kiungo wa Simba, Abdulhalim Humud, ameamua kuchukua uamuzi mgumu wa kusitisha rasmi mkataba wake
wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo.
Humud alitua Simba msimu uliopita
akitokea Azam na kusaini mkataba wa miaka miwili lakini mambo yalimuendea
tofauti baada ya kukosa namba kwenye kikosi cha kwanza huku akisugua benchi
mara kwa mara na wakati mwingine kutojumuishwa kabisa kwenye kikosi cha
wachezaji 18 kwa ajili ya mechi husika.
Pamoja na hayo, Humud amelifungukia
mengi Championi Jumatatu kuhusiana na hatua yake hiyo ya kuvunja mkataba huku
akiapa kutorudi tena Msimbazi katika maisha yake ya soka yaliyobaki.
“Sikushinikizwa na mtu kufikia hatua
yangu hiyo ya kuvunja mkataba na Simba, bali ni maamuzi yangu mwenyewe, sikuwa
na wakati mzuri muda wote nilipokuwa Simba tangu awali mpaka niliporudi kusaini
mwaka jana.
“Nimeangalia na kuona kwamba sikuwa na
thamani Simba ingawa mimi nilikuwa nikiithamini na kuipenda kwa moyo wangu
wote, nikagundua kuwa sikupaswa kuichezea Simba kwa kuwa sifaidiki na chochote.
“Sina haja ya kufafanua sana kilichokuwa
kinaendelea kuhusu maisha yangu na Simba kwa sababu kila kitu kipo wazi kwamba
klabu ilikuwa haihitaji msaada wangu wa uwanjani na mimi shida yangu ni kucheza
mpira na si kukaa benchi na kusubiri mshahara tu.
“Nimefanya hivyo si kwa nia mbaya bali
nimeangalia mustakabali wa maisha yangu ya soka pia, nimeona kabisa kwamba kama
mlolongo huu ukiendelea basi nitaishia pabaya kwenye kipaji changu cha soka,
hivyo ni bora nijiengue na kuangalia mambo yangu mengine,” alisema Humud
aliyewahi kukipiga Mtibwa na Azam.
“Niliwafuata viongozi na kuwaambia suala
hili kama wiki mbili zilizopita, nashukuru kwamba wamenielewa na kunionyesha
ushirikiano wa kutosha na juzi Jumamosi wakanikabidhi barua yangu ya kusitisha
mkataba wangu wa mwaka mmoja uliobaki.
“Na baada ya hapa si kwamba nitaichukia
Simba, hapana bali nitaendelea kuipenda lakini suala la kurudi kuichezea kwa
mara nyingine tena hilo halitawezekana katika maisha yangu yote ya soka
yaliyobaki,” alisema.
0 COMMENTS:
Post a Comment