May 5, 2014




FAMILIA ya Floyd Mayweather kwa hapa nyumbani unaweza kuifananisha kabisa na ile ya Matumla, iliyojaa mabondia wengi wenye vipaji kuanzia babu, baba hadi wajukuu na ikiwezekana hata kina dada.

Mayweather Jr ndiye bondia mwenye uwezo mkubwa kuliko wengine wote hadi sasa kwa kuwa hajapigwa hata pambano moja. Jana alfajiri amecheza pambano lake la 36 na kushinda huku akiweka rekodi ya kushinda 26 kwa KO.

Pambano lake dhidi ya Francos Maidana wa Argentina, limezua gumzo kwamba Muargentina huyo alishinda. Lakini takwimu zinaonyesha Maidana alirusha ngumi nyingi sana lakini hazikuwa na shabaha huku Mayweather akifanya vizuri zaidi na majaji watatu, wawili wakampa ushindi yeye na mmoja akasema ni sare.

Lakini gumzo kubwa kuhusiana na Mayweather ni mtu anayelipwa fedha nyingi zaidi kuliko binadamu mwingine yeyote kutokana na kazi anayoifanya.
Katika pambano la jana alfajiri dhidi ya Maidana amelipwa dola milioni 32 (zaidi ya Sh bilioni 51), maana yake fedha hizo amelipwa kwa muda wa dakika 36 tu.
akiwa mazoezini na baba yake mzazi

Katika ndondi kila raundi ni dakika tatu na wanapigana raundi 12 na inawezekana kama atafanikiwa kumdondosha mpinzani wake basi hawezi kufikisha dakika hizo. Unaweza kusema ndani ya saa moja anaingiza kitita cha pauni milioni 32, si mchezo.
Mcheza gofu maarufu Tiger Woods, amekuwa akilipwa hadi zaidi ya dola milioni 24, kila anapotwaa taji, hali iliyomfanya kuwa mwanamichezo anayelipwa zaidi.
Lakini kwa mwenendo wa Mayweather sasa, ndiye anachukua fedha nyingi kwa kuwa hata malipo yake yanajumuisha muda mchache anakuwa ameishajikusanyia mamilioni hayo ya fedha ambayo kuna wanamichezo wanacheza hadi kufikia kustaafu lakini hawapati hata robo ya fedha hizo.
Kitita cha dola milioni 32 si kikubwa zaidi kwake kulipwa, amewahi kulipwa hadi dola milioni 50 alipopambana na Robert Guerrero na akachukua dola milioni 41.5 alipomtwanga Cabero Alvarez.
Utajiri:
Mayweather ni bilionea ambaye utajiri wake sasa unafikia dola milioni 350 alizopata kupitia mchezo wa ngumi na hasa za kulipwa kabla ya pambano la jana alfajiri. Lakini mkali huyo anayetokea Las Vegas, Nevada nchini Marekani amewekeza kwenye maisha ya kifahari zaidi.
Anamiliki zaidi ya magari kumi ya kifahari kama Lamborghini, Bugatti, Ferrari na mengineyo tena mengi yakiwa yametengenezwa kutokea kiwandani na kuwekewa jina lake kabisa.
Pia anamiliki zaidi ya nyumba mbili za kifahari, nyumba yake ya Las Vegas ni kati ya zile za hali ya juu zaidi zinazolimilikiwa na wanamichezo kutokana na kuwa na mpangilio wa kifahari zaidi.
Kuonyesha kweli yeye ni tajiri, Mayweather ameweka rekodi ya kutorudia viatu vya kawaida vya kuvaa kwa miaka mitatu na nusu sasa. Maana yake hivi, kila akivaa kiatu kinakuwa kipya na vinatengenezwa na kampuni yake.

Kampuni:
Hana mkataba na kampuni yoyote ya michezo kama Adidas, Puma au Nike, badala yake anatumia kampuni anayoimiliki ya The Money Team au TMT. Ndiyo imekuwa ikidhamini baadhi ya mapambano yake.
akiwa na walinzi wake...

Kampuni hiyo inatengeneza nguo na viatu mbalimbali na inamfanya aweke rekodi ya kuwa mwanamichezo maarufu duniani ambaye hadhaminiwi na kampuni kubwa za vifaa vya michezo kama Nike, Adidas na nyingine. Hapo awali aliwahi kudhaminiwa na Reebok.

Wasanii:
Ni kati ya wanandondi wenye urafiki mkubwa na wasanii mbalimbali wa muziki na waigizaji kutoka Hollywood nchini Marekani.
Kwa sasa Justin Beiber na Lil Wayne ndiyo watu wake wa karibu zaidi. Awali alikuwa rafiki wa karibu wa 50 Cent lakini ilielezwa walitibuana sababu ya kugombea mwanamke na 50 ndiye alishikwa kwa usaliti.

Maisha:
Pamoja na utajiri wake mkubwa, Mayweather amekuwa akisisitiza kwamba kamwe maisha yake hayajawa rahisi kama watu wengi wanavyofikiri na mara nyingi amemlaumu baba yake mzazi, Mayweather Sr hadharani kuwa amekuwa tatizo.
Mayweather amewahi kutumia madawa ya kulevya kama ilivyo kwa mama yake na baba yake pia ambaye alikuwa muuzaji mkubwa na amekuwa akikubali kweli aliuza kwa lengo la kuisaidia familia yake na hata Mayweather alikuwa akipata fungu lake.
Lakini baada ya kuona baba mzazi anaishi katika maisha yasiyoeleweka, akaamua kumpeleka mwanaye akaishi kwa mama yake, yaani bibi yake na Mayweather ambaye alimlea.
Katika mahojiano kuhusiana na maisha yake, Mayweather amewahi kusema hivi: “Nimeishi maisha ya shida sana wakati nikiwa mdogo, chumba kimoja tulikuwa tunalala watu sita na hata hakukuwa na umeme, hauwezi kuamini.
“Wakati nilipokuwa narejea nyumbani ilikuwa kawaida kuona sindano zilizotumika kwa ajili ya matumizi ya madawa ya kulevya. Pia mama yangu mdogo alifariki dunia kutokana na HIV na hii ilitokana na kuchangia sindano wakati wa kutumia madawa hayo.”

Bibi:
Pamoja na mambo yote kuhusiana na kipaji chake, hasa kwa baba yake kujisifia yeye ndiye alifanya kazi ya kumpeleka gym, Mayweather anasema hakumbuki kuona baba yake akimpeleka kwenye sehemu ya starehe au hata kununulia ice cream tu.
Kuhusiana na suala la kipaji chake, basi anaamini bibi yake ndiye alikigundua hata kabla ya baba yake na baba zake wadogo wawili ambao walikuwa mabondia pia.
Anasema: “Ilifikia wakati nataka kuachana na mambo ya bondia ili nitafute kazi kwa kuwa tayari maisha yalikuwa magumu. Lakini bibi alinisisitiza kwamba nisifanye hivyo, niendelee kupambana kwa juhudi kwa kuwa nina uwezo mkubwa wa mchezo huo.
“Ilikuwa inashangaza kumsikia bibi anasema vile, nilitulia na kutafakari, nikaona ilikuwa ni sahihi kuendelea na kweli nikaongeza juhudi. Bibi ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuona uwezo wangu.”

TAKWIMU:
AMECHEZA  AMESHINDA   KO     SARE   KUSHINDWA
   46                            46               26         0                0
AMECHEZA RAUNDI      MIKANDA         AMEINGIZA
               351                                8                dola milioni 382

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic