DEWJI |
Na Mwandishi
Wetu
KASSIM Dewji
anayeaminika ni katibu mkuu mwenye mafanikio ya juu zaidi katika klabu ya Simba
ameibuka na kutoa siri kuwa kuna viongozi waliuza viwanja viwili mali ya klabu hiyo.
Dewji
aliyeiongoza Simba kuitoa Al Ahly mwaka 2003, amesema Simba ilikuwa na viwanja
vinne katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam, lakini viongozi waliokuwa
madarakani miaka ya 1980, waliviuza.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Dewji alisema alifanya uchunguzi wakati
akiwa katibu mkuu na kugundua suala hilo kwamba ilifanyika hujuma hiyo.
“Baada ya
hapo nikalazimika kutafuta mwekezaji kwa ajili ya kujenga kile kiwanja kingine
ambacho kilikuwa wazi na yamewekwa makontena tu. Pia tayari jiji lilianza
kutishia kukipora kwa madai kuwa hakiendelezwi.
“Jengo
ambalo mwekezaji alilijenga ndiyo lile lenye maduka, linajulikana kama Jengo la
Dewji na linaiingizia Simba shilingi milioni 180 kwa mwaka,” alisema.
Akizungumzia
uchaguzi wa Simba, Dewji alisema hataki kumpigia mtu kampeni badala yake
anawaasa Wanasimba kuwa makini zaidi.
“Wanasimba
wanajua nani wamchague, lakini lazima wawe makini na waangalie watu
wanaowachagua huko nyuma wamefanya nini.
“Maana
wengine wana kesi, hawakuwa waadilifu au walikwama kwenye taasisi waliokuwa
wanaziongoza. Wasiruhusu waingie na kuivuruga Simba, kweli kabisa kama
wanahitaji msaada wangu, mimi nipo ingawa msitegemee kuwa ninataka uongozi,”
alisema.
Dewji
alisisitiza kukubali viongozi wasio waadilifu kuchukua madaraka Simba ni sawa
na kuingamiza kwa miaka mingine minne ijayo.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment