Na Saleh
Ally
MAMBO ya
mpira yana burudani zake, lakini kuna sehemu bila ya kujali ni nani
anayehusika, lazima kuwe na suala la umakini mkubwa kuhakikisha mambo
yanavyokwenda.
Niwakumbushe,
ambao hampendi kuambiwa ukweli poleni lakini wakati maandalizi ya uchaguzi wa
Simba yanaanza kuna vitu vimeanza kujitokeza ambavyo vinaonyesha kabisa kuwa
hakutakuwa na umakini mbele.
Mambo hayo
ndiyo yanayopaswa kukemewa mapema kabisa ili kuhakikisha Simba inapata viongozi
sahihi ambao wataikomboa kutoka ilipokwama sasa na kuonekana si Simba tena
yenye makali badala yake ni myama mkali anayeweza kuchezewa sharubu na yeyote
yule.
Wakati
alipokwenda kuchukua fomu mgombea wa kwanza wa urais, Evans Aveva wanachama
walijitokeza kwa wingi sana na kusababisha aweke rekodi mpya ya kuwa aliyesindikizwa
na mashabiki na wanachama wengi sana huku akifunga baadhi ya mitaa ya Kariakoo
jijini Dar es Salaam.
Siku
iliyofuata, Michael Wambura naye akaenda kuchukua fomu ya urais pia. Wanachama
na mashabiki kibao wakajitokeza kumsindikiza, wakiwa wanacheza na kuimba kama
ilivyokuwa kwa Aveva ingawa hakufikia ile rekodi ya watu wengi kama
walimsindikiza Aveva siku moja kabla.
Katika siku
hizo mbili za kipimo kikubwa cha Simba inaelekea wapi, kuna mambo yamejitokeza
ambayo kama yataendelea, basi Simba itadidimia zaidi kuliko hata kipindi cha
Ismail Aden Rage ambaye anaondoka na kuiacha ikiwa sawa na timu ya ‘daraja la
nne’.
Moja:
Jambo la
kwanza ambalo ni dira mbaya kuelekea kwenye uchaguzi ni kuwa na watu wepesi,
wanaoweza kununuliwa au walio tayari kuiona Simba inaangamia kwa sababu ya njaa
au matumbo yao.
Mfano mzuri
ni kikundi cha kina mama pamoja na mashabiki kadhaa ambao walimsindikiza Aveva,
siku ya kwanza. Walionekana ni wenye furaha, walicheza kwa juhudi na kukata
mauno hadi wakaonekana burudani ya aina yake.
Kwa
kuwaangalia kwa mara ya kwanza, wanaonyesha walikuwa wakifurahia ujio wa Aveva
na kama ni wanachama maana yake wangempa kura. Lakini ajabu, watu haohao
wakaonekana katika tabasamu lilelile, wakicheza kwa juhudi kama siku iliyopita,
safari hii wakimpigia debe Wambura!
Sijui kama
Aveva na Wambura walilijua hilo au nao waliingizwa mjini na watu hao, lakini
hiyo ni dalili mbaya. Viongozi hao wawili ni wanachama wa Simba, hivyo lazima kuwe
na chaguo kwa kuwa hakuna mwenye uwezo wa kupiga kura kuchagua watu wawili
kushika kiti cha urais. Kura itaharibika.
Sasa hao
kina mama na wenzao, vipi leo wanaingia na Aveva kwa mbwembwe, na kesho ngoma
na miondoko ileile wanaingia wakiwa na Wambura. Jibu hao ni Simba wa kukodi!
Jiulize,
kama kuna Simba wa kukodi, maana yake inawezekana kununua kura? Je, kuna
wanachama walio tayari kuchagua yoyote hata kama Simba itadidimia ili mradi wao
watapata chao cha kunywa maji ya kunywa kwa siku tatu, nne au tano na klabu
hiyo kongwe ikapata mateso kwa miaka minne? Jibu liko wazi, tuwasiliane.
Ila naweza
kuweka msisitizo katika hilo, mara kadhaa nimekuwa nikiasa kwamba wanachama
ndiyo wamekuwa tatizo kupiga kura kishabiki bila ya kutafakari maneno ya
wagombea. Au tamaa zao, halafu mwisho ndiyo wanaolalamika uongozi haufai,
vizuri kujitathmini kwa kuwa sasa ndiyo wakati mwafaka.
Pili:
Baada ya
Aveva kuchukua fomu akisindikizwa na umati mkubwa, kilichoshuhudiwa siku hiyo
ni watu wakiimba na zaidi walizungumza kuwa Aveva ndiye mgombea sahihi na
mkombozi.
Siku
iliyofuata, mambo yalikuwa tofauti kidogo na idadi kubwa ya mashabiki
inawezekana wakiwemo wale waliokuwemo wakati Aveva akienda kuchukua fomu siku
iliyopita walikuwa wamebeba mabango yaliyojaa kashfa lukuki kwa watu mbalimbali
wa Simba.
Mfano lile
lilokuwa likisema Friends of Simba ni wezi, hawana pa kuiba zaidi ya Simba.
Mengine yalimnanga Katibu Mkuu wa zamani wa Simba, Kassim Dewji na kadhalika.
Ukiangalia
mabango yale kwa kuwa yaliingia na Wambura, maana yake ndiyo mpango wa timu ya
uchaguzi ya mgombea huyo ambayo imeamua kwenda na mwendo huo.
Hakika si
mwendo sahihi, kwa kuwa ni mwendo unaozidi kuifanya Simba ididimie kwa kuwa
kipindi hiki klabu hiyo inatakiwa kumrudisha kundini karibu kila aliyekuwa
mbali kutokana na uongozi mbovu uliopita.
Sidhani kama
Dewji anastahili kulaumiwa sana kwa kuwa Aveva wala Wambura hakuna aliyewahi
kufikia mafanikio yake akiwa Simba. Hadi leo kuna jengo ambalo linaingiza kodi
na mamilioni kwa klabu hiyo na baadhi ya viongozi bado wamekuwa wakizila,
kumbukeni lilijengwa wakati wa uongozi wake.
Achana na
hivyo, kama unazungumzia Friends of Simba, ndilo kundi ambalo kila linapokuwa
karibu na timu hiyo linaifanya kuwa bora zaidi na hata wakati inafika fainali
ya Caf mwaka 1993, huku ikiing’oa Zamalek na kuivua ubingwa wa Afrika, hao
Friends of Simba walikuwa karibu na Simba.
Anavyoingia
Wambura maana yake tayari ametengeneza vita na FOS, Dewji na wengine ikiwa na
maana hivi, Simba itaendelea kuwa kwenye makundi na migogoro. Rekodi zinaonyesha
hakuna timu imewahi kufanya vizuri ikiwa katika kipindi kama hicho.
Waliobeba
mabango kama walifanya hivyo kwa sababu ya posho wamuogope Mungu, lakini
Wambura kama aliona hiyo ni njia sahihi, namkubusha haiwezi kuwa bora badala
yake kwa uwezo alionao anaweza kujenga hoja na kutangaza sera.
Wanasimba
wanahitaji sera zaidi, wanataka mtu atakayewaeleza kuwa ana mipango gani, nini
tatizo na aalitatua vipi kwa kushirikiana nao. Lakini si kuanza na kuzodoa
watu, kutengeneza mapambano dhidi ya mtu na mtu.
Kama ni
maendeleo, basi yanapatikana kwa watu kuunganisha nguvu na si kutanguliziana
kashfa na dharau, Simba haitabadilika hata ashinde nani. Imani yangu akishinda
mmoja kati yao wagombea hao wawili, mmoja atakuwa tayari kumsaidia mwenzake
kuisaidia Simba, lakini kwa alivyoanza Wambura, maana yake ni tatizo!
0 COMMENTS:
Post a Comment