JUHUDI za Liverpool kuchukua ubingwa katika
hatua za mwisho za Ligi Kuu England zimeishia njiani katika hatua za mwisho
kabisa baada ya kuzidiwa pointi mbili na Manchester City.
Hilo limewaumiza mashabiki wengi wa timu
hiyo waliokuwa wanataka kukata kiu yao kutwaa ubingwa huo.
Lakini kwa viongozi wa Liverpool bado wana
furaha kutokana na kikosi chao kuwa chenye mapato ya juu zaidi kwenye Ligi Kuu
England kupitia kwenye malipo ya runinga.
Kawaida timu za England au kokote soka
lilipopiga hatua zaidi wamekuwa wakitegemea kujiendesha kupitia fedha za
viingilio uwanjani, wadhamini na malipo kutokana na haki za televisheni.
Kwa msimu wa 2013-14, Liverpool ndiyo
wamekuwa vinara baada ya kuingiza pauni milioni 99 ambazo ni za juu zaidi
kuliko klabu nyingine yoyote kati ya zile 20 zilizoshiriki ligi hiyo.
Manchester City ambao wamekuwa ndiyo
mabingwa wamepata kitita cha pauni milioni 98 ikiwa ni tofauti ya milioni moja
na walyopata Liverpool.
Chelsea nayo imejitutumua kwa pauni milioni
94 na kushika nafasi ya tatu kwa mapato ya fedha zilizotokana na ligi kama
ilivyo kwenye msimamo. Pauni milioni 93 kwa Arsenal, nafasi ya nne kama kwenye
msimamo pia.
Kila mechi moja ambayo huonyeshwa ‘live’,
timu inaingiza pauni milioni 6.5, pia inaweza kushuka au kupanda kutokana na
mkataba unavyoeleza kuwa itaonyeshwa katika nchi au mabara mangapi na maendeo
yapi.
Kawaida kila timu inashiriki Premiership
hupata kitita cha pauni milioni 54 kwanza na baada ya hapo mgawo unategemea na
mechi ngapi za timu ipi huonyeshwa kwa wingi.
Mfumo wa ugawaji uko hivi, zinachukuliwa
fedha zote zinazotolewa na wadhamini kwa ajili ya ligi, asilimia 50
zinagawanywa kwa timu zote, halafu baada ya hapo kunakuwa na mgawo wa pili.
Ile asilimia 50 ya pili nayo inagawiwa kama
ifuatavyo, asilimia 25 ya kwanza inagawiwa kwa timu kulingana na inakuwa katika
nafasi ya ngapi hadi mwishoni mwa ligi.
Halafu asilimia 25 ya mwisho, yenyewe
inagawiwa kwa kuangalia timu imeonyeshwa mara ngapi katika runinga. Hivyo hapa
ndipo Liverpool imeipita Man City kwa kuwa ina mechi ningi zaidi
zilizoonyeshwa.
Ndiyo maana utaona, hata Man United ambayo
imepata nafasi ya tano kwa kupata fedha nyingi za udhamini wa malipo ya runinga
wakati ipo katika nafasi ya saba.
Mechi 760 huchezwa katika Premiership, kila
timu kati ya 20 ikicheza mechi 38 na 154 pekee ndiyo huonyeshwa kupitia vituo
mbalimbali vya runinga duniani.
0 COMMENTS:
Post a Comment